WANAFUNZI na walimu wa Chuo cha Jamia Ahmadiyya Tanzania kilichopo mkoani Morogoro wamechangia kutoa damu salama chupa 59 kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu wenye uhitaji wakiwemo akina mama wajawazito wanaohitaji kufanyiwa upasuaji, watoto na wanaopatwana majanga ya ajali .
Mkufunzi wa Chuo cha Jamia Ahmadiyya Tanzania ,Shamuni Juma amesema hayo katika taarifa ya Chuo hicho kwa mgeni rasmi, Amiri na Mbashiri Mkuu Tanzania , Sheikh Khawaja Muzaffar Ahmad wakati wa mahafali ya 13 ya mwaka huu (2024).
Jumla ya wahitimu13 wakiwemo watatu kutoka nje ya nchi wakiwemo wawili kutoka Kenya na mmoja kutoka Burundi walitunukiwa Stashahada ( Diploma ) ya Theolojia katika masomo mbalimbali ya dini ,na lugha ya Kiingereza.
Juma amesema katika huduma ya kuchangia damu salama ilifanyika kwa nyakati tofauti ambapo awamu ya kwanza wanafunzi na walimu walichangia kutoa chupa 30 na awamu ya pili kwa kushirikiana na Shirika la humanity first walichangia chupa 29 za damu salama .
Naye Mkuu wa Chuo hicho na Naibu Amiri, Sheikh Abid Mahmood amesema ,Chuo kinaendeshwa na Jumuiya ya Waislamu wa Ahmadiyya kwa ajili ya kuwaandaa watalaamu na wasomi wanaokwenda kufundisha maadili mema katika jamii ya kiislamu ya Ahmadiyya na nyinginezo.
Mkuu wa Chuo hicho amesema licha ya kutoa elimu ya kidini, Jumuiya ya Ahmadiyya inajihusisha pia na kutoa huduma za kijamii zikiwemo za elimu, afya ,maji pamoja na uwezeshwaji umeme wa jua maeneo ya vijijini ambako hakuna huduma hiyo.
Kwa upande wake Amiri na Mbashiri Mkuu Tanzania, Sheikh Ahmad amewasihi walimu na wabashiri waliohitimu ya kwamba wanapoenda kuhubiri wasieleze makosa ya madhehebu na dini mbalimbali , bali wajikite katika kuielezea dini yao ya Kiislamu.
“ Nawasihi msiende kueleza makosa ,aibu ama upungufu ya dini nyingine ,bali enendeni kueleza uzuri wa dini uliyonayo “ amesema .
Amiri na Mbashiri Mkuu Tanzania, Sheikh Ahmad pia amewataka wahitimu hao wawe na hurka njema ndani ya jamii na kwamba wanapaswa kufikiria kwanza kabla ya kuongea jambo ili kupima kwanza iwapo lina maslahi mapana katika jamii.
“ Uwe unadhibiti ulimi wako kikamilifu ,huwezi kuongea bila kufikiria kwamba ni sahihi ama sio sahihi nah ii ni muhumu sana pia “ amesisitiza Amiri na Mbashiri mkuu wa Tanzania.