“Jamii itambue mchango wa TMA”

KATIBU Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Profesa, Godius Kahyarara ameitaka jamii kutambua mafanikio ya Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) kikanda na kimataifa kwa kuwa inafanya kazi nzuri na inayoonekana.
Akizungumza katika maonesho ya Mkutano wa 16 wa Wadau wa Sekta ya Uchukuzi kuhusu Ufuatiliaji na Tathmini (16th JTSR) unaofanyika jijini Arusha, Prof Kahyarara amesema ili kueleza mafanikio hayo ni vyema TMA ikajipanga kuwa na vipindi katika televisheni katika kueleza mafanikio ambayo mamlaka inayapata.

Mkutano huo wa 16 wa Wadau wa Sekta ya Uchukuzi kuhusu Ufuatiliaji na Tathmini (16th JTSR) umehusisha maonesho ya shughuli zinazofanywa na taasisi zilizo chini ya sekta ya uchukuzi.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu TMA ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Miundombinu na Ufundi, Dk Pascal Waniha, akaeleza kuwa TMA imekuwa kielelezo bora katika ukanda wa Afrika Mashariki pamoja na nje ya Kanda.

“Kazi kubwa imeendelea kufanyika katika kuiwakilisha nchi vizuri kwenye masuala ya hali ya hewa kimataifa na kueleza kuwa imeteuliwa na WMO kuwa muandaaji wa mafunzo ya rada katika Kanda ya Afrika yanayoratibiwa na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO).
Fursa hii imepatikana kutokana na uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya hali ya hewa unaoendelea kufanywa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.” Alisema Dk Waniha.

Mafanikio mengine yaliyoelezwa mbele ya Katibu Mkuu kupitia mabango ni pamoja na maendeleo katika shughuli za uangazi, ununuzi wa vifaa na mitambo ya hali ya hewa, udhibiti wa huduma za hali ya hewa pamoja na njia mbalimbali zinazotumika katika kusambaza taarifa za hali ya hewa kwa jamii na kwa sekta mahsusi.



