JAMII imeshauriwa kuacha matumizi ya pombe, tumbaku, sigara na ulaji wa vyakula vya sukari kwa wingi ili kuepukana na matatizo ya kinywa na meno.
Dk Matilda Mlangwa, Mkuu wa Skuli ya Kinywa na Meno MUHAS ametoa ushauri huo leo katika Maadhimisho Siku ya Afya ya Kinywa na Meno yenye kauli mbiu ‘Kinywa cha Furaha ni Mwili wa Furaha’ iliyofanyika katika jengo la Dental ndani ya Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Akizungumza na baadhi wa wananchi wa wanafunzi waliojitokeza eneo hilo Dk Mlangwa amesema katika kuadhimisha siku hiyo ni muhimu jamii ikazingatia afya ya meno kwani changamoto zake zinatibika licha ya kwamba zinaweza kusababisha ulemavu au kifo.
Amesema baadhi ya watu wanashindwa kupata tiba kutokana na ufahamu mdogo wa masuala ya meno hivyo wakati mwingine inaweza kusababisha shida ya saratani ya mdomo.
“Ni bora kusafisha meno mara mbili kwa siku, ikishindikana mara moja kwa ubora, sambamba na hilo pia kudumisha usafi wa meno,” amesema Mlangwa.
Naibu Makamu Mkuu wa Muhas, Emmanuel Balandya amesema chuo hiko kiko mbele katika kutoa elimu inayohusu afya ya meno kuendana na mahitaji.
Amesema chuo hicho kimekuwa kikitoa watalamu wa meno kwa miaka mingi hivyo ameshauri watu kuwa na tabia ya kufanya uchunguzi mara kwa mara.