Upandaji miti ni uhai wa mazingira

WASWAHILI husema, “Mchumia juani, hulia kivulini,” wakimaanisha kuwa mafanikio huletwa na juhudi. Methali hii inaakisi umuhimu wa upandaji miti katika jamii ili kujipatia manufaa ya kivuli, mvua, pamoja na mazingira salama.
Jamii nchini imetakiwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za upandaji miti ili kusaidia utunzaji na uhifadhi wa mazingira ambayo kwa sasa yanakumbwa na changamoto nyingi zikiwemo mmomonyoko wa udongo na mafuriko.
Akizungumza na HabariLEO, Mratibu na Katibu wa shirika la Environment is Life, Gerald Muunga, amesema miti ina faida nyingi kwa jamii na hivyo wananchi wanapaswa kujenga utamaduni wa kuipanda na kuitunza. “Miti ni tiba, lakini pia hutoa kivuli, husababisha mvua, huzuia mmomonyoko wa ardhi pamoja na mafuriko. Tunapaswa kuwekeza kwenye upandaji miti ili kuhakikisha mazingira yetu yanabaki salama,” amesema Muunga.
Kwa upande wake, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kupitia Ofisi ya Kinondoni, wamehimiza jamii kujitokeza kuchukua miti kwa ajili ya kuipanda kwenye maeneo mbalimbali kama mashuleni, pembezoni mwa barabara na katika taasisi za dini. SOMA: Miti yatajwa kuwa kinga dhidi ya joto kali.
Kanuti Matasha, Askari Mhifadhi Mwandamizi wa Misitu Wilaya ya Kinondoni, amesema: “TFS Kinondoni tupo tayari kutoa miche bure kwa ajili ya kampeni ya upandaji miti. Tunakaribisha mashule, vyuo, na taasisi nyingine kuwasilisha barua zenye kuainisha idadi ya miche na eneo ilipotengwa kwa upandaji.”
Amesisitiza kuwa utunzaji wa mazingira ni jukumu la kila mwananchi na ushirikiano wa pamoja ndio utakaosaidia kudhibiti uharibifu wa mazingira nchini. “Utunzaji wa mazingira unaanza na mimi, wewe na yule. Sote tunapaswa kuchukua hatua sasa,” amehitimisha Matasha.



