Jamii yatakiwa kukemea uporaji haki kwa wanawake

MKUU wa Mkoa Kigoma, Thobias Andengenye ameitaka jamii kukataa tabia ya watu wenye uwezo wa kifedha kupora haki za wanawake na watoto kwenye mashauri mbalimbali yanayojitokeza dhidi yao ikiwemo unyanyasaji kingono na masuala ya kumiliki mali.

Andengenye alisema hayo katika akiwa katika kijiji cha Makere Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma  alipokuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani na kubainisha kuwa bado haki za wanawake na watoto zimekuwa zikikiukwa kwa misingi ya kuwapendelea watu wenye uwezo kiuchumi.

Mkuu huyo wa mkoa amepinga vitendo vya ukatili kwa wasichana na watoto ikiwemo kukatishwa masomo na kuozeshwa kwa wanaume wenye uwezo wa kifedha, wanaotoa ng’ombe mambo ambayo yanakatisha ndoto za wasichana.

Alisema serikali itaendelea kutekeleza maazimio ya Beijing, Mpango wa Maendeleo ya Taifa na mkakati wa serikali katika kuongeza kipato na kuinua uchumi wa wanawake ili kuwafanya wanawake kuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa taifa na katika kuondoa umaskini nchini.

Akisoma risala kwa niaba ya makundi mbalimbali ya wanawake yaliyohudhuria maadhimisho hayo, Zuwena Hussein alisema kuwa kusimamishwa kwa mikopo ya asilimia 10 kwa makundi maalum kumekuwa na athari kubwa katika kuwafanya wanawake na wasichana kujikwamua na umasikini.

Mwenyekiti wa Jumuia ya Wanawake wa CCM Mkoa Kigoma (UWT),Agripina Buyogera alisema kuwa bado vitendo vya unyanyasaji na ukatili wa kingono havijachukuliwa kwa unaostahili na kuendelea kuathiri maisha ya wanawake na wasichana mkoani Kigoma hivyo kuitaka serikali na vyombo vyake kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na hali hiyo.

Aidha Buyogera alisema kuwa serikali haina budi kurudisha mikopo kwa makundi maalum wakiwemo wanawake inayotolewa na halmashauri kwani mikopo hiyo imekua na mchango mkubwa katika kuinua uchumi na kipato cha wanawake na hivyo kuwafanya waondoke na utegemezi.

Habari Zifananazo

Back to top button