Jamii zatakiwa kuishi vizuri kulinda watoto
JAMII imetakiwa kuishi kwa upendo katika familia na kuzuia migogoro isiyo ya lazima inayosababisha watoto kukosa huduma muhimu za malezi na makuzi na kuchochea vitendo vya ukatili kwa watoto.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dk Dorothy Gwajima wakati akifunga Mkutano Mkuu wa Maofisa Ustawi wa Jamii nchini uliofanyika katika Shule ya Polisi (TPS) Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Dk Gwajima amewataka maofisa ustawi wa jamii kutoa elimu kwa jamii kuimarisha mahusiano kwani migogoro inasababisha baadhi ya watoto kufanyiwa vitendo vya ukatili na kwenda kuishi na kufanyakazi mitaani.
“familia ni taasisi inayowaandaa watoto na sehemu salama ya kuishi, kukua na kuwa raia wema wenye maadili na wazalendo watakaosaidia ustawi wa taifa lakini familia isipokuwa imara itasababisha migogoro, malezi duni yanayoleta athari katika makuzi na maendeleo ya awali ya watoto ikiwemo kufanyiwa vitendo vya ukatili majumbani na kwenye jamii,” amesema.
SOMA: Mkuchika awafunda wanafunzi maadili
Aidha amewapongeza maofisa hao kwa kujadili kuhusu kuwanusuru watoto wanaoishi na kufanyakazi mitaani na kuwataka waongeze nguvu za kuzuia ongezeko la watoto hao mitaani kwani huko ndiko wanapofanyiwa vitendo vya ukatili.
“Tusiwasubiri waende kufanyakazi mitaani ndiyo tuwanusuru kwa kuwarudisha maana tunapishana na wengine wanaenda mtaani, tujipange tunaenda vipi kuzuia wasitoke majumbani kabisa lakini haimaanishi wakae hapahapo wakati wanafanyiwa ukatili,” amesema Dk Gwajima.
Awali Kamishna wa Ustawi wa Jamii, Dk Nandera Mhando alieleza baadhi ya maazimio ya mkutano huo kuwa ni kila mkoa kuwasilisha takwimu za watoto wanaoishi nakufanyakazi mtaani, idadi ya watoto waliounganishwa na familia zao kwa zaidi ya asiliamia 50 na wamejipanga kupunguza idadi ya watoto hao.
SOMA: Samia asisitiza maadili bora kwa watoto