Mkuchika awafunda wanafunzi maadili
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu (Kazi Maalum) ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Newala Mjini, Kepteni mstaafu George Mkuchika amewataka wanafunzi nchini kuzingatia suala la maadili ili wapate matokeo mazuri kwenye masomo yao.
Akizungumza wakati wa mahafali ya kwanza ya kuhitimu darasa la saba yaliyofanyika katika shule ya msingi ya St. Mary’s iliyopo Halmashauri ya Mji Newala mkoani Mtwara, mbunge huyo amesema mtoto hata kama awe na akili kiasi gani kama hana maadili ya dini yake nidhamu itapungua.
‘’Hatuna budi kuwapongeza walimu, wanafunzi na wazazi mliyowaleta watoto hapa na tunasema ili mtoto asome vizuri lazima awe na uhiyari wa kutaka kusoma unaweza kumpata mtoto mwingine akawa na akili lakini hataki kusoma, nawapongeza kwa kukubali mazingira ya shule na niwaombe muendelee kudumisha ushirikiano uliyopo,” amesema Mkuchika.
SOMA: Samia asisitiza maadili bora kwa watoto
Mkuu wa Wilaya ya Newala mkoani humo, Rajabu Kundya amewaomba na kuwasihi wazazi wilayani humo kuendelea kushirikiana na walimu katika malezi ya watoto wao kwani haifai kuwatelekezea walimu watoto hao bila kufatilia mienendo yao na namna anavyopata elimu.
‘’Mzazi angalu jipe kazi mara moja kwa mwezi kuwasiliana na shule juu ya suala la elimu kwa watoto wetu, mwezi huu utakwenda utakutana na mkuu wa shule atakwambia yanayoendelea shuleni, mwezi ujao utaonana na mwalimu wa darasa atakwambie mwenendo wa mtoto darasani lakini mwezi ujao usiache kuja kumtafuta mwalimu wa somo ambalo mtoto wako hafanyi vizuri ili mushauriane namna bora ya kumsaidia mtoto katika utoaji wa elimu,’’amesema Kundya.
SOMA: Taasisi yabanwa mafunzo yanayokiuka maadili
Meneja wa shule ya St. Mary’s Debora Vita kutoka Shirika la Mariamu Mtakatifu Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Newala mkoani Mtwara amesisitiza suala la nidhamu na upendo kwa wanafunzi shuleni hapo halafu elimu inafata huku akiwataka watoto hao wanaoondoka kwamba nidhamu waliyoionyesha shuleni wakaiendeleze huko mbele wanakokwenda kwani wasiwaangushe wazazi.
‘’Lakini wazazi msiache kuwahimiza watoto sala na dua kwani tusipo wajenga katika misingi ya dini hata wasome wawe wanasayansi wazuri kama hawana Mungu hawatakuwa watoto wazuri, kwahiyo watoto wangu wapenzi naomba mkamtangulize Mungu kwanza,’’amesema Vita.