PWANI: MKUU wa Wilaya ya Bagamoyo, Halima Okash, ameagiza kufungwa kwa taasisi ya Mango Kinder iliyopo Kata ya Dunda wilayani Bagamoyo mkoani Pwani, baada ya kituo hicho kudaiwa kukiuka utaratibu wa leseni yake ya kutoa haki kwa watoto.
Pia ameagiza mmiliki wa taasisi hiyo ambaye ni Mtanzania Franky Silvester Neumann na wenzake akiwemo mkewe Franky ambaye ni raia wa Ujerumani, wahojiwe zaidi, wakituhumiwa kukusanya watoto zaidi ya 200 na kuwapa elimu juu ya masuala mbalimbali ikiwemo yaliyo kinyume na maadili ya Mtanzania.
Akizungumza mkoani Pwani, Okash amesema baada ya ukaguzi katika kituo hicho wamekuta zana mbalimbali ambazo waligundua watoto hao wanafundishwa vitendo ambavyo ni kinyume na maadili.
“Tumekuta zana mbalimbali, ambazo zimrtufanya kugundua watoto hawafundishwi maadili mema na mengi ya mambo wanayofundishwa ni mambo ya kijinsia, ambayo yanakiuka taratibu, mila na desturi zetu,”amesema Okash na kuongeza:
“Nimeelekeza kusitishwa kibali na leseni ya taasisi hii na wote wanaohusika na taasisi tutaondoka nao kwa ajili ya mahojiano na uchunguzi zaidi, lakini hili eneo halitotumika tena, hawa watoto tangu Novemba mwaka jana wanakuja hapa na watu hawatoi taarifa kwa wakati, utamaduni wa kwetu wanaenda kuubadilisha,”amesema.
Kituo hicho kinadaiwa kuwakusanya wanafunzi kuanzia saa nane mchana hadi saa 12 jioni na kuwapikia chakula kisha kuwafundisha masuala mbalimbali bila ya kibali.
Awali wakati wa mahojiano Franky amesema: “Mimi nilikuwa Ujerumani nikawaambia Tanzania nina watoto hali yao sio nzuri, wakanipa ufadhili Euro 1000 kila mwezi tuwe tunawapikia watoto chakula, wakimaliza wanasoma msomo mbalimbali,”amesema.