Japan kuna soko la chai – Balozi Luvanda

BALOZI wa Tanzania nchini Japan, Balozi Baraka luvanda amekutana na wadau wa chai hapa nchini na kuwataka kujipanga kunufaika na soko la uhakika la chai nchini Japan.

Balozi Luvanda ametoa rai hiyo alipokutana na wadau hao katika kikao kilichoandaliwa na Bodi ya Chai Tanzania(TBT) na balozi huyo kwa lengo la kuziangazia fursa za chai nchini Japan.

Kikao hicho ni mwendelezo wa harakati za TBT za kuzifungua fursa za soko la chai ya Tanzania kwenda kila kona ya dunia ambapo TBT chini ya uongozi wa Kaimu Mkurugenzi, Beatrice Banzi ilienda kutafuta masoko ya chai nchini Japan.

Advertisement

Balozi Luvanda amesisitizia kuwa soko la chai la Japan ni kubwa na Tanzaniia inaweza kunufaika na soko hilo kwa kupeleka chai yenye ubora stahiki.

Katika hatua nyingine Balozi Luvanda ameitaka TBT kuhakikisha kuwa wakulima wa chai wa hapa nchini wanaongeza uzalishaji wa zao la chai kwa kuzingatia ubora na kwa wingi ili kukidhi soko la chai la nchini japan linalokadiriwa kuwa na watu milioni 125.

SOMA: Wizara ya kilimo yafungua fursa kilimo cha Chai

“Natambua namna ambavyo Bodi ya Chai mnavyozitangaza fursa za chai na ile ziara ya Japan imekuwa na mafanikio kwa sasa wawekezaji wanalenga kuja nchini kuwekeza kwenye zao la chai,” amesema Luvanda.

Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Chai Tanzania, Beatrice Banzi amesema zao la chai linazalisha wastani wa tani 26-27 elfu za chai kwa mwaka ikiingizia nchi wastani wa Dola milioni 50 na kutoa ajira wakulima wanaokadiriwa kufikia 32000

Amesema,”Chai ya Tanzania inauzwa zaidi katika nchi za China , Kenya , German, Japan , Nchi za Falme za Kiarabu, Uingereza na Vietnam.”

Mkurugenzi msaidizi upande wa mazao kutoka Wizara ya Kilimo ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu- Kilimo kwenye kikao hicho, Justa Katunzi amewataka wakulima wa chai kuhakikisha wananufaika na kilimo cha umwagiliaji.