‘Jengeni misingi ya haki, demokrasia kuelekea uchaguzi mkuu’

DAR ES SALAAM; VYOMBO vya habari nchini vimekumbushwa wajibu wao kujenga misingi ya haki na demokrasia kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Aidha, jamii imetakiwa kuzingatia maadili kwa watoto wakati wa malezi ili kujenga taifa lenye wataalamu imara kuliko sasa vijana wengi hawana umahiri kazini.

Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa alisema waandishi wa habari na wamiliki wa vyombo vya habari wana dhamana kubwa kuimarisha misingi ya demokrasia na haki.

“Tuchukue hatua kuhakikisha jamii inachopokea ni habari zilizopimwa na kuchujwa na ninyi wanahabari. Media mpo kuzihakiki hizo taarifa, kuondoa habari feki na kutoa zilizo sahihi kuekelea uchaguzi mkuu,” alisema.

Alikuwa akifungua mkutano wa wadau wa habari wakiwemo wamiliki wa vyombo vya habari, wahariri na wahadhiri wa vyuo vikuu vya habari ulioandaliwa na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika Tawi la Tanzania (MISA TAN) na Taasisi ya WAN IFRA, Dar es Salaam juzi.

Alisisitiza ubunifu na umakini kwa wanahabari wanapoandika na kutekeleza majukumu yao na kuwakumbusha kusimamia maadili ya taaluma yao, misingi, sheria na kanuni zinazowagusa.

“Tupo kwenye jamii ambayo inatafuta habari za kufurahisha, utani si za uchumi, maendeleo, hii inafanya watu wadhani media sasa ni kwa umbea, vichekesho tu,” Onesmo.

Alitaka vyombo vya habari vitengeneze ajenda kwa jamii kwa kuilisha habari zenye ukweli ili kuendelea kujenga imani na matokeo chanya katika changamoto za habari za uongozo zinazosambazwa kupitia mitandao ya kijamii na kasi ya matumizi ya akili mnemba.

Katika mijadala iliyofanyika katika mkutano huo, wahadhiri na wahariri walionesha ipo haja kwa jamii kurejea kwenye malezi wakisisitiza ndio chanzo cha wanafunzi wengi wanaohitimu vyuo kushindwa kuwa mahiri kitaaluma kazini.

Mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) ambaye pia ni mmoja wa wahariri wa Clouds Media Group (CMG), Joyce Shebe, akichangia mjadala alitaka nguvu kubwa iwekwe kwenye malezi na uchumi imara wa vyombo vya habari.

Mhariri wa Habari wa Mwananchi, Lilian Timbuka aliwkaumbusha wahadhiri kutekeleza utaratibu wa kupita kwenye vyombo vya habari kabla ya kufundisha ili wajue tansia inahitaji nini ili kuzalisha wataalamu wa habari kwa tija kwani kwa sasa hali si nzuri kwa wanafunzi wa vitendo.

Mhadhiri wa Shule ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Egbert Mkoko alisema tofauti kubwa inayojitokeza sasa kwa baadhi ya wahitimu wa vyuo kutokuwa mahiri kazini si makosa ya walimu ni matokeo ya malezi.

“Lazima tujiulize tulipoangukia, tumesikia mjadala hapa lawama zinaweza kuwa nyingi kwa wahadhiri, lakini kila mtu hapa anahusika, mtoto anajengewa uwezo kuanzia akiwa mdogo, turudi kwenye malezi,” alisema Dk Mkoko.

Mhadhiri wa SJMC, Dk Dotto Kuhenga akitoa mada kuhusu uhimilivu na ustahimilivu wa vyombo vya habari, alihimiza ubora wa maudhui, ubunifu, teknolojia na uchumi imara kama njia za vyombo hivyo kudumu.

Mwenyekiti wa MISA TAN, Edwin Sokko alieleza dhamira ya taasisi hiyo kuendeleza mijadala na elimu kwa wanahabari kuongeza weledi katika taaluma.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button