JK: Niliwekeza kwenye mkongo kukabili rushwa

RAIS mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete amesema aliamua kuwekeza kwenye Mkongo wa Taifa ili kupambana na rushwa.

Kikwete amesema hayo jijini Arusha jana asubuhi alipozungumza kwenye Kipindi cha Power Breakfast kilichorushwa na Kituo cha Redio cha Clouds cha Kampuni ya Clouds Media ya Dar es Salaam.

Kiongozi huyo aliyeiongoza Tanzania kuanzia mwaka 2005 hadi 2015, alikuwa Arusha kuhudhuria mkutano wa wadau wa demokrasia Afrika.

“Shabaha yangu kubwa ilikuwa kupambana na rushwa, unajua mkifika mahali ambapo mtu kutafuta huduma katika ofisi za serikali halazimiki kwenda mpaka kwenye dirisha kwenye ofisi ya mtu, mnakuwa mmepiga hatua kubwa,” alifafanua Kikwete.

Alitoa mifano ya faida za mkongo kuwa umewezesha huduma utoaji leseni, tiba na elimu kutolewa kidijiti hivyo kuondoa mianya ya kuomba au kutoa rushwa kwa kuwa hata malipo yanafanywa kidijiti.

“Inarahisisha maisha, lakini ni mojawapo ya hatua muhimu katika kupambana. Na mimi ile naita rushwa sumbufu, ni zile ambazo watu wanahitaji huduma wanazungushwa, wanazungushwa, lakini mkifika mahali mimi nataka leseni ya biashara unakwenda kwenye website (tovuti), unatuma maombi yako, wanakujibu, unatakiwa kulipa fee (ada) kiasi hiki, na wewe unatumia siku yako unalipa kwenye halmashauri…watu wanaitazama demokrasia kwenye kupiga kura tu, hapana,” alieleza Kikwete.

Aliongeza: “Mkiwa na serikali mnaendesha kidigitali mnapunguza rushwa…maana kuna zile rushwa za kwenye mikataba, lakini rushwa nyingine zinazosumbua watu ni hizi za huduma mbalimbali.”

Alisema wazo la kuwa na Mkongo wa Taifa alilipata akiwa Marekani akiwa kwenye harakati za kuishawishi moja ya kampuni binafsi kuja kuwekeza kwenye Reli ya Kisasa (SGR).

Alisema alioneshwa michoro pamoja na mtandao wa nyaya, na akaelezwa ni ‘taarifa bomba’ hivyo wanaweza kuutoa Afrika Kusini hadi Pwani ya Mashariki, na kama angekuwa tayari Dar es Salaam iwe kituo.

Alieleza kuwa baada ya kukubaliana na wazo hilo, aliamua kuwekeza kwenye Mkongo wa Taifa na alizungumza na China wakatoa mkopo.

“Kwanza nilihakikisha nafanya mpango hizi nchi jirani kama Burundi, Congo ile ya Mashariki, Zambia, Malawi, Uganda na Rwanda tunaziunganisha kwetu kwa sababu wakitumia wanalipa. Tutakuwa wapuuzi sisi Mungu ameweka nchi yetu kijiografia halafu hatuutumii kunufaika nayo, jiografia hapa tulipo ni rasilimali,” alisema Kikwete.

Alisema suala la serikali kujiendesha kimtandao lina faida nyingi ikiwamo watu kupata haki zikiwamo za kidemokrasia kwa wakati zikiwamo za mahakamani na utawala bora kwa ujumla.

“Unajua demokrasia ni dhana pana, mara nyingi watu wanabaki kuzungumzia uchaguzi tu, lakini demokrasia ina masuala ya utawala bora, haki za msingi za raia… lakini maendeleo ya kidigitali yana faida zake…mfano mkishajiunga kidigitali mtu popote alipo anaweza kupiga kura,” alifafanua Kikwete.

Aliongeza: “Sasa hivi mahakamani wanaendesha kesi kidigitali, lakini zamani ilikuwa mpaka wamalize waandike hukumu kwa kalamu, lakini siku hizi hukumu ikishaisha unachapishiwa inatoka…hiyo yote ni demokrasia.”

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x