JKCI waendesha uchunguzi, matibabu bure sherehe za Uhuru

DAR ES SALAAM: WATU 182 leo Desemba 9, 2024 wamepata huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kambi maalumu ya upimaji iliyofanyika katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group, ikiwa ni maadhimisho ya miaka 63 ya Uhuru wa Tanganyika.
Upimaji huo umefanyika bila malipo yoyote yale katika hospitali hiyo iliyopo eneo la TAZARA jijini Dar es Salaam, ambapo watu wazima waliopata huduma walikuwa 147 na watoto 35.
Akizungumza kuhusu upimaji huo, Kaimu Mkurugenzi wa JKCI Hospitali ya Dar Group, Dk.Tulizo Shemu amesema kati ya watu wazima 147 walioonwa 72 walikutwa na matatizo mbalimbali ya moyo ikiwemo shinikizo la juu la damu, matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo na kutanuka kwa kuta za moyo.
Kwa upande wake daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto kwenye hospitali hiyo, Eva Wakuganda ametoa wito kwa wananchi kuwa na tabia ya kuchunguza afya zao, kwani magonjwa ya moyo wakati mwingine yanaweza yasioneshe dalili.

Ameshauri jamii kufanya uchunguzi wa magonjwa hayo kwa watoto wao, kwani dalili zao zinaweza kuwa zile za kutoongezeka uzito, kupumua kwa shida, kutoka jasho jingi wakati wa kunyonya, kuchoka, kubadilika rangi na kuwa wa bluu, pamoja na moyo kwenda mbio ama wakati mwingine magonjwa hayo kuwa kimya hivyo kutoonesha dalili.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi waliofika katika kambi hiyo wamempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fursa za uchunguzi wa afya kwa wananchi wa Tanzania.
Jonson Makona, mkazi wa Mbezi Luis amesema vijana wengi siku hizi wamekuwa waoga kujitokeza kufanya uchunguzi wa magonjwa yasiyoambukiza, lakini yeye amewiwa kupima afya ili awe na uhakika wa maisha kwani magonjwa ya moyo yanawapata watu wote na sio wazee tu.



