NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dk Khatibu Kazungu amesema mradi Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (JNHPP) ambao unaingiza zaidi ya megawati 1000 kwenye Gridi ya Taifa ni chachu kubwa katika kukuza uchumi.
Dk Kazungu amesema hayo leo Desemba 28, 2024 alipotembelea eneo la mradi, Rufiji mkoani Pwani na kushuhudia kazi kubwa inayoendelea kufanywa na Wizara ya Nishati kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
“Mradi huu ni kielelezo muhimu sana katika nchi yetu kwani moja ya chachu kubwa za kukuza uchumi nchini ni matumizi ya umeme, kuna uhusiano mkubwa wa umeme na maendeleo ya kiuchumi na mifano halisi tunaiona, nchi nyingi duniani zenye matumizi makubwa ya umeme zimeendelea sana kiuchumi, amesema Kazungu.
Aidha, amemsisitiza mkandarasi wa mradi kumaliza kazi kwa wakati na kuwapongeza Tanesco kwa usimamizi wa mradi huo.
Vilevile ameitaka Tanesco kugeukia vyanzo vingine vya umeme kama jotoardhi na jua ili kuhakikisha kunakuwa na umeme wa kutosha kwa matumizi ya ndani ya nchi na pia kuwezesha biashara ya umeme nje ya nchi.
Maendeleo ya jumla ya mradi wa JNHPP hadi kufikia Novemba 30 2024 yamefikia asilimia 99.55 na kuingiza 1,175 MW katika Gridi ya Taifa. Mradi wa JNHPP una uwezo wa kuzalisha megawati 2,115.