Jokate – Nimejipanga kushirikiana na viongozi, wanachama
Ni baada ya kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu UWT
KOROGWE, Tanga: Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Jokate Mwegelo amesema ameupokea kwa unyenyekevu mkubwa na furaha kubwa uteuzi huo na kusisitiza kuwa amejipanga kushirikiana na viongozi na wananchama wote wa UWT.
Mwegelo ameandika mengi katika ukurasa wake saa chache baada ya Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM kuteua kushika wadhifa huo baada ya kutumikia serikali kwa miaka kadhaa kama Mkuu wa Wilaya Kisarawe, Temeke na Korogwe.
“Nitumie nafasi hii kuishukuru Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM chini ya Mwenyekiti wake na Rais wetu Mpendwa Dkt.
Samia Suluhu Hassan kwa kuniteua kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania ngazi ya Taifa.
“Ni heshima kubwa kuona Chama changu kikiendelea kutuamini Vijana na kutupa majukukumu makubwa ya kukitumikia Chama na Taifa. Naamini uteuzi huu utakuwa chachu kwa Mabinti wadogo Chipukizi wa Chama kupambania ndoto zao wakiamini wanacho Chama ambacho kinawajali na kuwaamini watu wote wenye uwezo na dhamira ya kweli ya kuleta mageuzi ya kweli na maendeleo ya Chama na Taifa letu,” ameandika Jokate.
Jokate amemshukuru Mwenyezi Mungu, Familia yake, na Wananchi wa Korogwe kwa kumuombea na kumshika mkono. “Nimepokea meseji na simu nyingi za pongezi, nimezisoma pia comments zenu nzuri mitandaoni, nawashukuru sana.”
Amesema: “Nimejipanga kushirikiana na Viongozi na Wanachama wenzangu wote wa UWT kote nchini kwa uadilifu, ueledi, ubunifu, ustadi, uzalendo, umakini nikitanguliza mbele maslahi mapana ya Chama na Taifa ili kuendelea kuiimarisha Jumuiya yetu na kukijenga Chama chetu.”
Aidha, nipo tayari kushirikiana na Wadau wote wanaopigania Maendeleo na Ustawi Wanawake kote Duniani bila kujali tofauti zetu za Itikadi za Vyama, Dini, Utaifa, Kabila.