Jukwaa kujadili mustakabali wa viongozi

DAR ES SALAAM: Jukwaa la Uongozi wa Wanawake ni muhimu katika kujadili namna ya kuhakikisha wanawake wanaopata nafasi za uongozi wanadumu katika nafasi hizo na kuendelea kutumia uzoefu wao kuchangia maendeleo ya jamii hata baada ya kumaliza vipindi vyao vya uongozi, amesema Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Uongozi (Uongozi Institute) Kadari Singo.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika Jukwaa la Uongozi wa Wanawake Singo amesema pamoja na kuongezeka kwa uwakilishi wa wanawake katika Bunge na taasisi mbalimbali bado kuna haja ya kuweka mifumo itakayowawezesha kuendelea kushiriki katika uongozi baada ya kumaliza muda wao wa kuhudumu hususan wanawake wanaoingia Bungeni kupitia viti maalumu.

Amesema changamoto hiyo inaibua maswali kuhusu namna ya kuwafuatilia wanawake wanaomaliza vipindi vyao vya uongozi kuwasaidia kurejea katika nafasi nyingine na kutumia maarifa pamoja na uzoefu walioupata kwa manufaa ya taifa badala ya kupoteza mchango wao baada ya kuondoka katika nafasi hizo.

Singo amebainisha kuwa mafanikio katika kuongeza idadi ya wanawake wanaoshika nafasi za uongozi hayapaswi kupimwa kwa uwakilishi pekee bali pia kwa uwezo wa kuwawezesha kudumu katika nafasi hizo na kuendeleza safari zao za uongozi.

Amesisitiza umuhimu wa kuondoa vikwazo vya kimuundo na kitaasisi vinavyoweza kukatiza maendeleo ya wanawake katika uongozi.

Aidha amesema jukwaa hilo linatoa fursa kwa washiriki kujadili uzoefu wa wanawake viongozi kutoka Tanzania Afrika na maeneo mengine duniani pamoja na kujifunza matokeo ya utafiti kuhusu njia za kuimarisha ustahimilivu na mwendelezo wa uongozi wa wanawake nchini Tanzania.

Ameeleza kuwa kupitia majadiliano hayo, washiriki wanatarajiwa kupendekeza suluhisho za vitendo ikiwemo mifumo ya ushauri uelekezaji wa kitaaluma kujengeana mitandao na kuandaa njia zitakazowawezesha wanawake kuendelea kukua na kushika nafasi za juu za uongozi katika sekta za umma, binafsi na taasisi za kijamii.

Katika hatua nyingine Singo amesema Taasisi ya Uongozi inaendesha programu ya miezi sita ya kuwaandaa wanawake wa Afrika walio katika ngazi za kati na za juu za uongozi, kwa kuwapatia mafunzo ushauri na uelekezaji kutoka kwa wataalamu wa uongozi na mabadiliko kutoka maeneo mbalimbali duniani.

Amesema programu hiyo inalenga kuwasaidia washiriki kuelewa changamoto zinazowakabili wanawake viongozi kutambua uwezo wao wa kiuongozi na kuandaa mipango ya maendeleo binafsi itakayowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Singo ameongeza kuwa katika makundi manane ya awali ya programu hiyo wanawake 399 wamehitimu kati ya takribani 400 waliokuwa wameshiriki hatua inayoonesha umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika programu zinazojenga uwezo wa wanawake na kuimarisha mitandao yao ya kitaaluma.

Amesisitiza kuwa jukwaa hilo ni sehemu muhimu ya kutafuta majibu ya changamoto zinazowakabili wanawake katika safari zao za uongozi kwa lengo la kuhakikisha kuwa mafanikio ya kupata nafasi za uongozi yanaambatana na uwezo wa kudumu kukua na kuendeleza mchango wao katika maendeleo ya Tanzania na Afrika kwa ujumla.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button