Kada za afya zenye mapungufu kupatiwa ufumbuzi

WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu amemwelekeza Katibu Mkuu Wizara ya Afya kufanya uchambuzi wa kina kwenye kada za afya kuanzia ngazi ya taifa mpaka zahanati ikiwemo kada ya wataalamu wa maabara ili kuweka kipaumbele sahihi katika kuajiri wataalamu wa kada zenye upungufu mkubwa kulingana na mahitaji ya nchi.

Waziri Ummy amesema hayo leo, Juni 19, 2023 akiwa anajibu hoja za wataalam wa maabara waliohoji mitandaoni kuhusu changamoto ya ajira za wataalam wa maabara zinazotolewa na wizara ya afya pamoja na ofisi ya rais TAMISEMI.

“Wataalam wa Maabara ni kada muhimu katika utoaji huduma bora za Afya, ni kweli kuwa tiba sahihi ya ugonjwa inategemea huduma za uchunguzi wa magonjwa (Maabara na Radiolojia),” Amesema Waziri Ummy.

Aidha, alisema muundo mpya unaotarajiwa kuanza Julai 1, 2023 utakuwa na Kurugenzi kamili ya huduma za uchunguzi (Directorate of Diagnostic Services) ambayo kabla ya hapo ilikuwa ni eneo (Section) chini ya idara ya huduma za tiba (Directorate of Curative Services).

Habari Zifananazo

Back to top button