KAGIS sasa yageukia wenye ulemavu michezoni

MRADI wa Kuwezesha Wasichana Balehe Kuendelea na Masomo (KAGIS), unaotekelezwa katika mikoa ya Geita na Kigoma sasa umeamua kugeukia kundi la watu wenye ulemavu ili kuwainua kupitia michezo.

Mradi wa KAGIS unatekelezwa na Shirika la Rafiki Social Development Organisation (RAFIKI SDO) kwa Ushirikiano na Plan International chini ya ufadhili wa serikali ya watu wa Canada (Global Affairs Canada).

Ofisa Mradi wa KAGIS kutoka RAFIKI SDO, Sabatho Simon ameeleza hayo katika mchezo wa soka kati ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu na wasio na mahitaji maalum uliochezwa uwanja wa Shule ya Msingi Mbugani mjini Geita.

Amesema ushiriki wa watoto wenye mahitaji maalumu kwenye michezo itasaidia kuchagiza maendeleo ya elimu jumuishi na kuhamasisha watato hao kupata fursa ya kuonesha vipaji nje ya elimu ya darasani.

“Lengo la kuwahusisha kwenye michezo hii, ni kwa sababu hawa walemavu ni wazazi wa miaka ijayo, kwa hiyo tunawaandaa na wao wajisikie kuwa ni wana jamii wanaweza pia kuwa na familia, ” amesema.

Amesema kupitia michezo pia itasaidia kuimarisha afya za watoto wenye ulemavu na kuambatanisha kampeni ya kuhamasisha wazazi kupeleka watoto wa kike shule iendane na kujumuisha wenye ulemavu.

Ofisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Mji wa Geita, Cathbert Byabato amesema halmashauri hiyo ina shule moja kwa watoto wenye ulemavu na shule zingine sita zinatoa elimu kwa walemavu kwa mfumo jumuishi.

“Kwa hapa kituo cha Mbungani wapo watoto wenye changamoto ya afya ya akili, walemavu wa viungo, wapo watoto wenye changamoto ya ngozi, wapo wenye usonji, viziwi na watoto wenye uoni hafifu.

“Tunaendelea kutoa msisitizo kwa wazazi na walezi kutambua watu wenye mahitaji maalum ama walemavu kuwa wanayo fursa sawa na watoto ambao hawana mahitaji maalum,” amesema.

Mwanafunzi mwenye mahitaji maalumu Shule ya Msingi Mbungani, James Andrea amesema kupitia michezo, KAGIS imewafanya wajione na wao wanayo nafasi ya kushindana na kuonesha vipaji vyao.

Habari Zifananazo

Back to top button