‘Kagueni migodi kwa faida, usalama zaidi’
DODOMA: WAKAGUZI wa migodi wametakiwa kuendelea kusimamia na kuimarisha kaguzi katika maeneo yao ya kazi ili sekta ya madini iendelee kukua na kuchangia asilimia 10 katika pato la taifa ifikapo mwaka 2025.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Msafiri Mbibo akimwakilisha Waziri wa Madini, Anthony Mavunde katika Mkutano mkuu wa mwaka wa Wakaguzi wa Migodi kutoka Tume ya Madini uliyofanyika leo Mei 30, 2024 katika Ukumbi wa Kambarage – Hazina jijini Dodoma.
Amesema, migodi ya madini 21,686 imekaguliwa katika kipindi cha Julai, 2023 hadi Aprili 2024 kati ya migodi hiyo, migodi mikubwa ni nane, migodi ya kati 56 na migodi midogo 21,622. Ukaguzi uliowezesha sekta ya madini kuendelea kuimarika na kuongeza makusanyo na mchango wake katika ukuaji wa uchumi.
“Pamoja na kuimarika kwa sekta ya madini na mchango wake katika ukuaji wa uchumi bado kuna changamoto za matukio ya ajali katika maeneo ya wachimbaji wadogo ambapo husababishwa na kuanguka kwa mashimo/maduara ya uchimbaji na ajali zingine husababishwa kwa kukosekana kwa hewa ndani ya mashimo/maduara,” amesema Mbibo.
Kutokana na hali hiyo, Tume ya Madini chini ya Katibu Mtendaji wake, Mhandisi Yahya Samamba imeagizwa kuimarisha na kuhakikisha ukaguzi unafanyika mara kwa mara hasa katika maeneo ya wachimbaji wadogo ambapo matukio mengi ya ajali yamekuwa yakitokea ukilinganisha na maeneo ya wachimbaji wa kati na wakubwa.
SOMA: Sh Trilioni 1 kibindoni sekta ya madini
Pia, wametakiwa kutoa elimu ya mara kwa mara kwa wachimbaji wadogo ambao wengi wana uelewa mdogo wa masuala ya afya mahala pa kazi na usalama.
“Hivyo mna wajibu mkubwa kuhakikisha mnawasimamia ipasavyo na kuwaelekeza njia salama za uchimbaji pamoja na matumizi salama ya baruti ili kuepuka ajali zinazohatarisha usalama wao na kurudisha nyuma jitihada za ukuaji wa sekta ya wachimbaji wadogo nchini,” amesema Mbibo na kuongeza,
“Sisi kama wizara tunaamini kuwa, uhai wa mchimbaji mmoja una umuhimu mkubwa kuliko uzalishaji wowote wa madini”.
Amesema, sehemu kubwa ya makusanyo yote ya Wizara ya Madini yanatokana na mrabaha na ada ya ukaguzi, hivyo migodi inaposimama kufanya kazi kutokana na ajali inaathiri makusanyo kwa wizara na serikali kwa ujumla.
Mbibo pia, amewaagiza wakaguzi wa migodi, kuimarisha kaguzi katika migodi yote mikubwa, ya kati na hususan migodi ya wachimbaji wadogo nchini ili kuepusha ajali zinazoweza kutokea na kusababisha kusimamisha uzalishaji.
“Mkaendelee kutoa elimu juu ya afya, usalama, matumizi salama ya baruti na utunzaji wa mazingira kwa wachimbaji wote nchini, niwasihi mkatekeleze majukumu yenu kwa badii kwa kuzingatia uadilifu, uwajibikaji na waledi, pasipo kujihusisha na vitendo vya rushwa na pasipo kumuonea mchimbaji yeyote, lakini pia kuendelea kushirikiana katika kutekeleza majukumu yenu ili kuweza kutimiza lengo,” amesisitiza Naibu Katibu Mkuu.
Naye, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba awali akizungumza amesema sekta ya wakaguzi wa migodi, baruti na vilipuzi pamoja na ukaguzi wa mazingira ndio injini ya Sekta ya Madini.
Amesema eneo la uchimbaji linapokosa usalama, afya, mazingira yanapoharibika ndio matokeo ya mwisho hayawezi kufakiwa.
Mhandisi Samamba amesema kuwa tangu Tume ya Madini ianzishwe mwaka 2017 na kuanza kazi rasmi Aprili 2018 takwimu za ajali kwa maana ya vifo, ajali na athari za mazingira zimepungua na kwamba namba hizo hazijapungua kwa bahati mbaya bali ni kazi kubwa inayofanywa na wakaguzi kwa niaba ya Tume na kwa kwa maelekezo ya Wizara ya Madini chini ya Waziri Anthony Mavunde
“Ukiachia mbali vita ambayo watu wengi wanakufa kwa mara moja watu 200 hadi 1,000 eneo lingine linalouwa watu wengi kwa mara moja ni eneo la uchimbaji, ikitokea madhara watu 40 hadi 50 hupoteza maisha kwa wakati mmoja,
“Nikuhakikishie kama Tume ya Madini tutaendelea kusimamia vizuri kupitia kwa wakaguzi wetu wa ndani,” amesema Mhandisi Samamba.
Aidha, amesema kuwa kikao hicho ni maalum kwa ajili ya kujengewa uwezo, kubadilishana uzoefu kwenye shughuli za usimamizi wa migodi nchini.