WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki amewataka waandaaji wa maonesho ya Utalii ya Kimataifa ya Swahili (SITE) kuyaboresha zaidi ili kupata washiriki wengi kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Hata hivyo ametangaza tarehe ya maonesho hayo ambayo yatakuwa nane kuwa ni Oktoba 11-13 mwaka 2024.
Kairuki amesema hayo wakati akihitimisha maonesho Dar es Salaam na kuwashukuru wadau walioshiriki kwenye maonesho hayo ambapo amesema bila ushiriki wao yasiingeweza kufanyika kwa kiwango na ubora mkubwa kama lilivyofanyika.
Vilevile ameipongeza Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa kupamba maonesho hayo kwa kuandaa bustani ya wanyamapori hai ambayo imekuwa kivutio kikubwa kwa waliotembelea.
Aidha amewaomba wadau kutoa maoni kuhusu maonesho hayo ambayo yatasaidia kuboresha maonesho ya mwakani na kuyafanya kuwa ya kimataifa.
“Maboresho haya yatatujenga na kutusaidia kutuingiza katika maonesho makubwa ya kimataifa kama vile world tourism Market.” amefafanua Kairuki
Kairuki amesema pamoja na kazi kubwa ya kuboresha miundombinu iliyofanywa na kusaidia kuleta watalii pia alifafanua kuwa ongezeko kubwa la watalii nchini limetokana na kazi nzuri iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kupitia filamu ya “The Royal Tour” ambayo ilionyeshwa katika vituo vingi vya televisheni vinavyotambulika nchini Marekani na kwingineko duniani ili kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania.
Comments are closed.