Kamati yaridhishwa upatikanaji maji Hanang

MANYARA: KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira imeridhishwa na mpango wa kurejesha huduma ya maji safi na salama katika maeneo yaliyoathirika na maporomoko Wilaya ya Hanang mkoani Manyara.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jackson Kiswaga amesema hayo walipotembelea maeneo yaliyoathiriwa na maporomoko ya tope wilayani Hanang mkoani wa Manyara.

Amesema wamejionea na kuridhishwa na kazi ya kurejesha miundombinu iliyofanywa kwa haraka iliyogharimu Sh bilioni 9 za serikali.

Advertisement

“Ari na kasi ya utendaji kazi iendelee tunataka azma ya Rais Samia Suluhu Hassan ya upatikanaji wa maji safi na salama ya kufikia asilimia 85 vijijini na asilimia 95 mijini itimie ifikapo 2025,” amesema Kiswaga.

Kwa kujibu wake kamati itakwenda kusukuma fedha katika miradi ambayo imeshaanza lakini haijapata fedha ili iweze kukamilika kwa wakati.

Ziara ya kamati hiyo imetokana na maombi ya Mbunge wa Jimbo la Hanang, Samwel Hhayuma ya kuitaka kamati kuona hali ya huduma ya maji katika maeneo yaliyoathirika na maporomoko ya tope na mpango wa kurejesha huduma Wilaya ya Hanang.

Awali Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew amefafanua kuwa zaidi ya miradi minne ya maji iliharibiwa wilayani Hanang na miradi miwili katika mji wa Katesh kufuatia maporomoko ya tope.

Wizara ya Maji ilikuja na mpango wa dharura wa kuhakikisha inapatikana njia ambayo wananchi walioathiriwa wanapata maji.

“Sambamba na adha hiyo nalipongeza sana bunge tumepitia mpango wa Dira ya Taifa ya mwaka 2050 hiyo ndio dira ambayo itaenda kubainisha mipango ya wizara ya maji hivyo tumeendelea kutekeleza miradi ya kimkakati,” amesema.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga ameeleza kuwa mkoa umefanya kazi nzuri ya utekelezaji wa miradi ya maji tangu Rais Samia alipoingia madarakani ambapo upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi umeongezeka na kufikia mijini asilimia 84 na vijijini asilimia 71.

Aidha amebainisha kuwa Manyara ina asili ya kifugaji na baadhi ya  maeneo ni makame ambayo hayapatikani maji kwa urahisi hivyo kupitia miradi ya maji inayotekelezwa inasaidia upatikanaji wa maji safi na salama.

Akitoa taarifa ya mkoa kuhusu huduma ya maji Meneja wa Wakala wa Maji Mijini na Vijijini (RUWASA)  Mkoa wa Manyara, James Kionaumela amefafanua kuwa mpango wa dharura wa muda mfupi na muda mrefu umetumika kurejesha huduma ya maji katika maeneo yaliyoathiriwa na maporomoko.

Mpango huo ni pamoja na uchimbaji wa visima virefu 15 ambapo visima 9 vikipata maji na 6 haikupata maji.