Kambi kusaidia watoto, vijana wenye kigugumizi yaja

CHAMA cha Mtindo Maalumu wa Uzungumzaji Tanzania (CHAMMUTA) kitaanza kambi maalumu ya watoto wenye kigugumizi itakayofanyika Dar es Salaam, lengo ni kuwahudumia watoto na vijana kuzungumza kwa kujiamini.

Kambi hiyo itaanza Juni 23 hadi 27 mwaka huu na inatarajia kupokea watoto kati ya 30 na 50 wenye kigugumizi.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mratibu wa kambi hiyo, Dudley Mbowe alisema watoto wenye kigugumizi wanahitaji mazoezi ya kuzungumza kwa kujiamini, ushauri wa kitaalamu kutoka kwa wanasaikolojia na wataalamu wa mawasiliano na kuwajengea uwezo wa kuwa mabalozi wa kuielimisha jamii kuhusu kigugumizi.

Mbowe alisema kaulimbiu ya kambi hiyo ni: ‘Ota, zungumza, ishi’ inayolenga kuhamasisha watoto na vijana kutambua ndoto zao, kuzungumza kwa ujasiri na kuishi maisha kamili bila woga wala aibu.

“Tunaamini kuwa kila mtoto au mtu ana haki ya kusikilizwa, kueleweka na kuheshimiwa bila kujali changamoto yake ya maisha ikiwemo kigugumizi,” alieleza.

Mwanzilishi na Mwenyekiti wa chama hicho, Ally Baharoon aliyataka mashirika ya kijamii, sekta ya afya na elimu, sekta binafsi, wahisani, wazazi na walezi wa watoto wenye kigugumizi kushiriki kambi hiyo.

Alisema kupitia kambi hiyo, wanatarajia kuleta mabadiliko chanya kwa watoto, vijana na watu wote na kuwajengea hali ya kujiamini na kuwa sehemu ya jamii inayoelewa, kukubali na kusaidia maendeleo ya watu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button