WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro anatarajia kuzindua Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal AID Campaign ),kwa mkoa wa Morogoro Desemba 13.
Mkuu wa wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala amesema hayo leo Desemba 12 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wake utakaofanyika Manispaa ya Morogoro.
Amesema kampeni imejikita katika kutoa elimu ya kisheria kwa wananchi hususan katika masuala ya ukatili wa kijinsia, migogoro ya ardhi, mirathi, usuluhishi wa migogoro kwa njia mbadala, na masuala yahusuyo haki za binadamu kwa ujumla.
SOMA: Kampeni msaada wa kisheria ya Mama Samia kutua Moro
Mkuu wa wilaya amesema lengo kuu la Kampeni ni kulinda na kukuza upatikanaji wa haki kwa wote kupitia huduma ya msaada wa kisheria nchini.
Amesema katika kufikia lengo hilo, kampeni inaongeza uelewa wa kisheria na haki za binadamu kwa jamii hususan haki za wanawake na watoto na inatoa huduma ya ushauri wa kisheria na unasihi kwa waathirika na manusura wa ukatili wa kijinsia.
Pia kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu elimu ya sheria, masuala ya haki na wajibu na misingi ya utawala bora.
“Kampeni hii imebeba maono ya Rais wetu Dk Samia Sululu Hassan ya kutoa huduma na kuwafikia wananchi wanyonge wakiwemo wanawake na watoto” amesema Kilakala.
Mkuu wa wilaya amesema baada ya kampeni hiyo kuzunduliwa itaendelea katika ngazi ya halmashauri zote tisa za mkoa huo katika kata kumi kwa kila Halmashauri na Mitaa/Vijiji vitatu kwa kila Kata.
“ Natoa wito kwa wananchi wa mkoa wetu kuitumia vema fursa hii adhimu ya kushiriki uzinduzi huo na hatimaye kupata elimu ya msaada wa kisheria na kuzitatua kero na migogoro yap bila malipo yoyote” amesema Kilakala.
Kampeni hiyo inafanyika kwa miaka mitatu kuanzia Machi, 2023 hadi Februari, 2026 katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Utekelezaji wake ulianza mkoani Dodoma Mei 28, 2023 baada ya kuzinduliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa , Mei 27, 2023 mkoani humo.