Kampeni “Tuwaambie Kabla Hawajaharibiwa” yazinduliwa 

KATIKA jitihada za kuzuia mmomonyoko wa maadili na kuwalinda watoto na vijana dhidi ya ukatili wa kijinsia na athari za utandawazi, Mkoa wa Iringa umezindua kampeni kabambe ya “Tuwaambie Kabla Hawajaharibiwa.”

Kampeni hiyo inayolenga pia kuelimisha wanafunzi wa shule za msingi hadi vyuo vikuu kuhusu madhara ya tabia hatarishi kama vile matumizi ya dawa za kulevya, ulevi, na mapenzi ya jinsia moja, imezinduliwa leo katika viwanja vya Kichangani na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Peter Serukamba.

Akizindua kampeni hiyo iliyohudhuriwa na idadi kubwa ya wanafunzi, Serukamba, alisema kuwa ukatili wa kijinsia na utandawazi umekuwa na athari kubwa kwa watoto na vijana, kwani unaleta tamaduni ambazo hazina faida kwa jamii zetu.

“Kama Taifa, hatuwezi kumudu kuacha vijana wetu wakiharibiwa. Ni muhimu tuwazungumzie mapema kabla hawajaathiriwa na tabia zisizofaa,” alisema.

Serukamba alisema kampeni hiyo inalenga pia kuhakikisha vijana wanajenga tabia njema na kujitambua ili waweze kuchangia kwa tija katika ujenzi wa taifa.

“Tukiwaelimisha vijana wetu mapema, tunalinda kizazi chetu kijacho na tunajenga Taifa lenye maadili thabiti,” alisema.

Mkuu wa Mashtaka wa Mkoa, Beatrice Nsana, alilipongeza Jeshi la Polisi, hasa dawati la jinsia, kwa kuongoza kampeni hii kwa bidii akisema; “Kwa ushirikiano na mahakama, tutahakikisha kuwa wahusika wa vitendo vya ukatili wa kijinsia wanachukuliwa hatua stahiki, na jamii ielimishwe ili matukio haya yapungue.”

Alisisitiza kuwa kila mmoja ana wajibu wa kuwalinda watoto dhidi ya madhara ya tamaduni mbaya na tabia hatari zinazowakumba.

Kamanda wa Polisi Mkoa RPC Allan Bukumbi alisema kampeni ya “Tuwaambie Kabla Hawajaharibiwa” imekuja kwa lengo la kuwatahadharisha dhidi ya tabia zinazoweza kuharibu mustakabali wao.

“Ni lazima tuweke mikakati na kutoa elimu stahiki ili kuwalinda watoto wetu dhidi ya athari hizi. Ni umuhimu pia kwa familia kuelimishwa ili iwe ngome ya kwanza katika mapambano dhidi ya mmomonyoko wa maadili,” alisema.

Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Iringa, Tiniel Mbaga, alizungumzia mkataba wa kimataifa dhidi ya ukatili wa kijinsia kwa watoto akisema serikali ya awamu ya sita imeweka sheria na miongozo thabiti ya kupambana na ukatili wa kijinsia.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada alizungumzia matarajio ya kampeni hiyo akisema itasaidia siyo tu vijana, bali pia wazazi na walezi katika kuhakikisha watoto wanalelewa katika mazingira salama.

Alitoa wito kwa jamii nzima kushirikiana ili kuzuia mmomonyoko wa maadili na kuhakikisha vijana wa Iringa wanalelewa katika mazingira yenye usalama na uadilifu.

Habari Zifananazo

Back to top button