Kampeni usafi awamu ya pili Dar yaja

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla leo ametangaza kuanza awamu ya pili ya kampeni ya Safisha Pendezesha Dar es Salaam, baada ya awamu ya kwanza ya kampeni hiyo iliyodumu kwa mwaka mmoja na miezi mitano kuwa na mafanikio makubwa ikiwemo kufanya jiji hilo kushika nafasi ya sita kwa usafi Afrika.

Akizungumza wakati wa kikao kazi cha tathimini Awamu ya Kwanza na kuweka mikakati ya awamu ya pili, Makalla ameelekeza watendaji kuanzia ngazi ya mkoa, wilaya, kata na mitaa kusimamia ufanyaji usafi.

Aidha Makalla amesema miongoni mwa mambo yayopaswa kuwekewa mkazo zaidi ni udhibiti wa ufanyaji biashara holela, usafishaji mazingira, upendezeshaji na upandaji miti kwenye bustani.

Kutokana na mwamko mkubwa wa usafi uliopo, Makalla ameelekeza kila halmashauri kushirikiana na wadau ambao wapo tayari kupendezesha jiji, huku akielekeza taasisi za TANROAD, TARURA na DAWASA kufanya kazi kwa ushirikiano.

Pamoja na hayo Makalla amesema lengo la kampeni hiyo ni kufanya Dar es Salaam izidi kushika nafasi za juu kwa usafi Afrika, jambo litakalosaidia kudhibiti pia mlipuko wa magonjwa  ikiwemo kipindupindu na hata kudhibiti maambukizi ya malaria.

Makalla ameendelea kusisitiza wananchi kufanya usafi kila ifikapo Jumamos ya mwisho wa mwezi, huku akiwataka wafanyabiashara kufanya biashara kwenye maeneo waliyopangwa.

Habari Zifananazo

Back to top button