Kampeni Usingizi wa Starehe kugawa vyandarua Mil.3.7

SERIKALI kwa kushirikiana na Marekani kwa pamoja wamezindua kampeni ya ugawaji wa vyandarua vyenye dawa kwenye kaya ikiwa ni jitihada za pamoja katika mapambano dhidi ya malaria nchini.

Kupitia kampeni hii inayojitambulisha kwa jina la Usingizi wa Starehe chini ya ufadhili wa Mfuko wa Rais wa Marekani wa kupambana na Malaria (PMI), itasambaza takribani vyandarua milioni 3.7 vyenye dawa katika kaya za mkoa wa Kagera na Tabora.

Akizungumza jana wakati wa hafla ya uzinduzi wa kampeni hiyo, Naibu Waziri wa Afya Dk Godwin Mollel alisema, serikali zote mbili zina furaha kufanya kazi kwa ushirikiano katika utekelezaji wa mradi huo lengo likiwa kuwalinda wananchi katika vita dhidi ya malaria na kupunguza vifo vitokanavyo na ugonjwa huo.

“Leo, tunasimama kwa pamoja katika dhamira yetu ya kupambana na ugonjwa wa Malaria nchini, kwa kuzindua kampeni ya ugawaji vyandarua vyenye dawa katika kaya za mkoa wa Kagera na Tabora.

“Tunatambua ushiriki wa washirika wetu, ikiwa ni pamoja na Serikali ya Marekani, pamoja wadau wengine wa maendeleo, katika juhudi zetu za pamoja za kupambana na malaria,” aliongeza.

Mshauri Mkazi wa Masuala ya Malaria kutoka Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), Naomi Serbantez alisema kwa kubadilisha vyandarua vilivyochakaa na kuhakikisha upatikanaji wa vyandarua vipya, kunaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa maambukizi ya malaria na kulinda afya za jamii nchini.

“Serikali ya Marekani inafurahi kuungana na wadau wetu wa malaria katika kuzindua kampeni hii ugawaji wa vyandarua vilivyotiwa dawa kwa jamii kwa kuhakikisha kuwa kaya zinapata vyandarua, na vyandarua hivi vinatumiwa kwa usahihi ili kupunguza kwa kiasi kikubwa maambukizi ya malaria na kuwalinda watu walio katika mazingira hatarishi,” alisema na kuongeza:

“Kupitia kampeni hii, Marekani inasisitiza dhamira yake ya kuendelea kuisaidia Tanzania katika mapambano dhidi ya malaria na kuboresha afya na ustawi wa raia wake.”

 

Habari Zifananazo

Back to top button