Kampeni ya kisheria yafanikiwa 95% Missenyi

KAGERA: KAMPENI ya msaada wa kisheria ya Mama Samia wilayani Missenyi mkoani Kagera imefanikiwa kwa asilimia 95.3 ndani ya siku 15.
Mafanikio hayo ni tangu ilipozinduliwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro Aprili 14 mwaka huu katika viwanja vya Mayunga Manispaa ya Bukoba.
Mratibu wa kampeini hiyo wilayani Missenyi Maxmillan Fransis alisema kuwa ndani ya siku 15 wilayani Missenyi tangu Aprili 15 hadi 28 ambapo kata zilizopangwa kufikiwa ni 15 na zote zimefikiwa na vijiji vilivyopangwa kufikiwa ni 43 na vilivyofikiwa ni 41.

“Kampeini imekuwa na mafanikio makubwa na mwitikio mkubwa sana ,mwanzoni ilikuwa iwe siku 10 lakini serikali iliongeza siku 5 kulingana na uhitaji wa wananchi ,tumefikia vijiji 41 na vijiji viwili ambavyo kampeini haikufanikiwa tulifika na viongozi wao walisema wanamisiba mikubwa , vingine vyote vimenufaika na kampeini hiyo”
Alisema kuwa kupitia kampeni hiyo makundi mbalimbali yalipata elimu yakiwemo ya boda boda ,wanafunzi ,wakulima,wazee,watu wenye ulemavu,taasisi binafsi ,waajiliwa serikalini huku elimu kuhusu umiliki wa ardhi, matumizi sahihi ya ardhi, wosia miradhi, ukatili ,matunzo ya watoto yakitolewa katika mikutano ya hadhara ili kunufaisha umma na kuwafundisha kufuata sheria.

Alisema kuwa migogoro iliyojitokeza kwa wingi ni migogoro ya ardhi ,mirathi na ukatili hivyo migogoro mingi imetatuliwa kwa njia ya usuluhishi na ambayo haijatatuliwa imekabidhiwa kwa vitengo ili kupatikana utatuzi wa kudumu .
Aidha migogoro ya kisheria kwa wananchi ambao hawana mawakili tayari mashauri yao yamekabidhiwa kwa mawakili ili kuwasaidia kuendelea na hatua za mahakama.

Akitaja mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kutoa elimu ya maswala ya kisheria ambayo imewezesha kufikia wananchi 14,020 kati ya hao wanaume ni 6,905 na wanawake ni 7,115
Aidha watendaji wa vijiji,kata,wenyeviti wa vijiji na vitongoji Madiwani wamejengewa uwezo juu ya maswala ya kisheria kutokana na kushughulikia kero za wananchi Kila siku ambazo zinahitaji utaalamu wa maswala ya kisheria .
Alitaja changamoto zilizojitokeza kuwa ni uwepo wa malalamiko ya muda mrefu kuhusu matumizi ya ardhi baina ya wananchi na serikali za vijiji, jambo ambalo limechochea uvunjifu wa amani na baadhi kugoma kuchangia maendeleo ya vijiji kwa sababu ya migogoro ya ardhi .



