DAR ES SALAAM: KAMPENI ya Msaada wa Kisheria wa Mama Samia imewahudumia wananchi 493,638 katika kipindi cha miezi 15 tangu kuanzishwa kwake na kufanikiwa kuwatoa mahabusu na wafungwa wapatao 7000.
Kampeni hiyo ina lengo la kulinda na kukuza upatikanaji wa haki kwa wote kupitia huduma ya msaada wa kisheria bila kujali uwezo wake wa kifedha, kampeni inayotambulika kama MAMA SAMIA LEGAL AID (MSLA).
SOMA: UN kuunga mkono Kampeni ya Mama Samia
Akiwa katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa yanayofanyika jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi na Mratibu wa Huduma za Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Ester Msambazi amesema tayari wameshaifikia mikoa saba ambayo ni Dodoma, Shinyanga, Manyara Ruvuma, Singida, Simiyu, na Njombe.
“Tunatekeleza Kampeni ya Msaada wa Kisheria kwa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, (Samia Suluhu Hassan) akitaka kuona kila aliyekosa uwezo wa kuweka wakili katika changamoto inayomkabili anasaidiwa na kupata haki yake,” amesisitiza.
Msambazi amesema katika mikoa hiyo saba wengi wa waliokutana nao ni wanaume ambao wanazidi laki mbili pamoja na kutoa vyeti vya kuzaliwa vipatavyo 5,200.
Amesema katika kufika mikoani humo kuwasaidia wananchi, kampeni hiyo imewajengea uwezo viongozi wa maeneo hayo katika kuwahudumia wananchi kwenye changamoto mbalimbali wanazokutana nazo.
“Lakini siyo tu kutoa elimu, siyo usajili peke yake, siyo kuwasaidia mahabusu na wafungwa, kupitia kampeni hii pia tunajenga uwezo kwa wadau mbalimbali kwa wasaidizi wa kisheria, watendaji wa kata, watendaji wa vijiji, waheshimiwa madiwani kuhusiana na masuala ya haki za binadamu,” amesema Msambazi.
Akizungumzia hali ya huduma kwennye Maonesho ya Sabasaba, Msambazi amesema watu 323,000 wamepatiwa huduma huku wakisajili migogoro 79.
“Kuna msemo wanasema kwamba wanaume huwa hawajitokezi, lakini katika kundi hili wanaume ni 222,000 pia tumesajili migogoro 79, ambapo migogoro mingi ikiwa ni ya ardhi na mirathi,” amefafanua.
Wananchi ambao wamefika kupata huduma katika banda hilo la MSLA akiwemo mama mjane Iluminata Msanta kutoka Tabata na kijana Wilson Rucho kutoka Segerea wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutambua adha wanazokutana nazo katika kupata haki zao.
Kampeni hii ambayo inafanyika kwa miaka mitatu imeanza Machi, 2023 na itamalizika Februari, 2026 katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.