UN kuunga mkono Kampeni ya Mama Samia

DAR ES SALAAM: KAIMU Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Msaada wa Kisheria ulio chini ya Wizara ya Katiba na Sheria, Ester Msambazi amesema, Umoja wa Mataifa (UN) umeonesha nia ya kuunga Mkono kile kinachofanywa na Kampeni ya Mama Samia Legal Aid (MSLAC) ambayo imekuwa ikitoa huduma ya msaada wa kisheria bure kwa wananchi.

Msambazi amesema imekuwa ni faraja kwa serikali kkuona kwamba kinachofanyika kwenye kampeni hiyo hata UN umekiona na kukithamini.

Advertisement

Akiwa kwenye Banda la Wizara ya Katiba na Sheria lililopo kwenye Viwanja vya maonesho hayo yanayofanyika Barabara ya Nyerere, jijini Dar es Salaam, Msambazi amesisitiza kuwa kampeni hiyo itaenda kwa kasi kwakuwa UN wataunga mkono juhudi hizo za Rais Samia Suluhu Hassan.

SOMA: Makanjanja kaeni chonjo msaada wa sheria wa Samia

“nimeona sasa tunaenda kuungwa mkono kwa kiasi kikubwa na kampeni itakimbia sana kwa sababu wao kuonesha wamethamini kampeni yetu, inamaana kubwa saana kwetu kwamba sasa tutakwenda kupata wadau wengi zaidi Umoja wa Mataifa UN watatuunga Mkono na tutafikia Wananchi kwa kiasi kikubwa kwa sababu masuala ya huduma kwa jamii, msaada wa kisheria sio suala la Serikali pekee yake,” amesema Msambazi.

Wananchi ambao wamepatiwa huduma katika viwanja vya sabasaba wamesema kampeni hiyo imekuwa msaada mkubwa hasa kwa watu wenye matatizo mbalimbali ya kisheria ambao hawajui waanzie wapi.

Lengo la MSLAC ni kuhakikisha kila mtu anapata fursa sawa katika mizania ya kisheria kwani huduma hiyo humuwezesha mhitaji asiyeweza kumudu gharama za wakili kupatiwa wakili wa kumsimamia kesi au shauri lake mahakamani. Pia huduma hiyo inatoa elimu ya sheria.