Kampeni zimeipa CCM ushindi – Nsokolo

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa Kigoma kimesema kuwa kampeni na mwenendo wa uchaguzi uliofanywa na chama hicho kupitia viongozi wake unawapa uhakika wa kushinda nafasi zote zinazogombewa katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27 mwaka huu.

Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo (CCM),Deogratius Nsokolo akizungumza na waandishi wa habari mjini Kigoma akitoa tathmini ya kampeni zilizofanywa na chama hicho  alisema kuwa chama kimefanya kampeni katika maeneo yote ya Kigoma kwa viongozi wa mkoa,wilaya,wabunge na madiwani kushiriki kikamilifu kuwanadi wagombea.

Nsokolo alisema kuwa katika mikutano hiyo viongozi hao wameeleza kazi kubwa iliyofanywa na Rais Samia katika kupeleka maendeleo kwa wananchi na hivyo kuwa na uhakika wa kushinda katika vijiji vyote 306 vya mkoa Kigoma ambavyo wamesimamisha wagombea wakiwa pia na wagombea 34 wa nafasi ya wenyekiti waliopita bila kupingwa pia kwenye vitongoji 1858 vya mkoa Kigoma wagombea wa nafasi ya mwenyekiti kwenye vitongoji  647 wamepita bila kupingwa.

Advertisement

Katika hatua nyingine chama cha ACT Wazalendo jimbo la Kigoma Mjini kimesema kuwa dua ya Ngamia iliyosomwa ikiongozwa na Kiongozi wa Chama Mstaafu, Zitto Kabwe inawapa Imani kwamba watashinda uchaguzi huo bila kutumia nguvu wakiamini hakutakuwa na wizi au udanganyifu wa kura utakaofanyika.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika viwanja vya kwa noti Ujiji mjini Kigoma Mwenyekiti wa Chama cha ACT jimbo la Kigoma Mjini, Halfan Bona amesema kuwa Pamoja na idadi kubwa ya wagombea wa nafasi ya Mwenyekiti kwa chama hicho kuenguliwa na msimamizi wa uchaguzi wamesema kuwa kwenye vijiji na vitongoji ambavyo wamesimamisha wagombea wana uhakika wa kushinda.

Mwenyeekiti huyo wa ACT jimbo la Kigoma mjini amewataka wanachama na wapenzi wa chama hicho kutofanya vurugu zozote kupigania matokeo bali wahakikishe wanapiga kura kwa kuchagua viongozi wa chama hicho na kumuacha Mungu awaongoze kwenye ushindi kwani Dua ya Ngamia waliyosoma kwa yeyote atakayewaibia kura itamdhuru.