Kampuni 35 zasajiliwa kununua pamba

DODOMA: ZAIDI ya kampuni 35 zimesajiliwa na kupewa leseni ya kununua pamba kwa utaratibu wa soko huru.

Mbunge wa Maswa Magharibi, Mashimba Ndaki (CCM) alitaka kujua, serikali inachukua hatua gani na madhubuti kuhakikisha kunakuwa na ushindani kwa Wafanyabiashara katika ununuzi wa Pamba.

Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde akijibu swali hilo alisema, ununuzi wa pamba nchini hufanyika kwa utaratibu wa soko huru ambapo zaidi ya kampuni 35 zimesajiliwa na kupewa leseni ya kununua pamba na usajili unaendelea ili kuongeza ushindani, kampuni hizi hununua pamba kulingana na hali ya soko ya msimu husika na bei dira iliyokubaliwa na wadau.

Aidha, Serikali husimamia na kuhakikisha bei dira iliyokubalika na wadau inazingatiwa katika ununuzi wa pamba.

Pamoja na utaratibu huo, bodi ya pamba imeingia mikataba na kampuni za ununuzi wa pamba ambao wameajiri maafisa ugani wanaotoa huduma za ugani katika kata zinazozalisha pamba kwa lengo la kuongeza tija na uzalishaji wa zao hilo.

Kampuni hizo zinapewa leseni ya kununua pamba katika Kata zilizoajiri Maafisa Ugani kulingana na bei dira inayokubaliwa na wadau kwa msimu husika kulingana na bei ya soko.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button