Kanisa kuendesha maombi kwa viongozi

Kanisa Dar kuendesha maombi kwa viongozi

MAOMBI maalum ya  kuwaombea viongozi wakuu wa nchi,pamoja na Tanzania kwa ujumla yanatarajia kuanza leo Jumatatu jijini Dar es Salaam.

Maombi hayo ya wiki moja yatakayoambatana na semina ya neno la Mungu, yameandaliwa na Kanisa la Calvary Tanzania Assemblies of God (CAG) ‘Chuo cha Manabii’, lililopo eneo la Bandari Kavu, Ubungo Maziwa, Dar es Salaam.

Akizungumza kanisani hapo jana, Katibu wa Kanisa hilo Lucas John, alisema maombi hayo ni sehemu ya kutimiza maandiko katika biblia.

Advertisement

“Maandiko katika waraka wa kwanza kwa Timotheo 2:1-2, Mungu ameliagiza kanisa kufanya maombi kwa ajili ya viongozi na wenye mamlaka, ili Taifa lidumishe upendo, amani na utulivu,” alisema na kuongeza kuwa:

“Kufanya hivi ni katika kutii agizo hilo pamoja na kutekeleza moja ya majukumu ya msingi ya kanisa letu.”

Katibu huyo alisema maombi hayo yataongozwa na Mchungaji Kiongozi wa Kanisa hilo, Imelda Maboya akishirikiana na viongozi wengine, yatafikia tamati Jumapili wiki hii.

“Tunawakaribisha watu kutoka sehemu mbalimbali jijini kuhudhuria maombi haya yatakayokuwa yakianzaa saa 11 jioni kanisani hapa,”alisema na kuongeza kuwa CAG ina makanisa zaidi ya 1,500 Tanzania Bara na Zanzibar.