Kapinga aipa FCC maagizo udhibiti bidhaa bandia

DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, ameiagiza Tume ya Ushindani (FCC) kuweka nguvu upya kuhusu udhibiti wa bidhaa bandia sokoni.
–
Pia ameitaka tume hiyo kuweka mifumo na njia bora za kupokea malalamiko kutoka kwa mlaji wa mwisho wa bidhaa au huduma ili kuongeza ufanisi na ulinzi.
–
Kapinga ametoa maagizo hayo wakati akizungumza katika Siku ya Maadhimisho ya Haki za Mlaji Duniani iliyofanyika leo Aprili 2, jijini Dar es Salaam.
–
Amesema mlaji ni mhimili muhimu katika ukuaji wa uchumi wa taifa, hivyo FCC ina jukumu la kumlinda na kuhakikisha malalamiko yao yanafanyiwa kazi kwa ufanisi.

“Serikali imeipa tume mamlaka ya kisheria kumlinda mlaji, kabla ya hapo lilikuwa jukumu la mahakama,” amesema Kapinga.
–
Kapinga ameitaka FCC kuhakikisha wakati mwingine wa maadhimisho hayo kunakuwa na wahusika (mlaji) na wadau wengine, ili kuwapa elimu na kuhakikisha uhusiano baina yao unaimarika.
Amesema kuwa suala la usalama wa bidhaa ni matokeo ya bora ya jamii salama, hivyo walaji wanapaswa kuwa makini.
“Mlaji anapaswa kuuliza maswali, ili kuwa na soko lenye uwazi na uwajibikaji,” ameongeza Kapinga.
Mwenyekiti wa Tume ya Ushindani (FCC) Dk Aggrey Kalimwage amesema tume ina haki na nguvu ya kushughulikia malalamiko ya mlaji kwa mujibu wa sheria, hivyo kila mlaji ana haki ya kupata bidhaa salama.
Amesema kuwa tume imejipanga kumhudumia mlaji na ili kufanikisha hilo, ushirikiano baina yao, wizara na idara zingine za udhibiti zinahitaji kuweka nguvu ya pamoja.
Dk Kalimwage amezungumzia pia jitihada za kudhibiti bidhaa bandia ambapo amesema tume imeendelea kuwajibika katika kufanikisha suala hilo.
“Katika kufanikisha hilo, tutachochea mapato, upatikanaji bidhaa salama, na kumlinda mlaji,” amesema Dk Kalimwage.
Aidha, Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Ushindani (FCC), Khadija Ngasongwa amesema wananchi wengi bado hawazifahamu haki za mlaji huku juhudi zikiendelea kuwapa elimu.
Amesema kutokana na changamoto hiyo, FCC imeendelea kutoa elimu hiyo kwa umma kuhusu haki na wajibu wa mlaji ili kuwawezesha kufanya maamuzi sahihi wanaponunua bidhaa na huduma.
Aidha, amesema taasisi hiyo imefanya kampeni za utoaji elimu katika mikoa ya Dar es Salaam na Njombe, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuwajengea uelewa kuhusu masuala ya ulaji na ushindani.



