Kapinga aipa tano ALAF

DAR ES SALAAM -WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amesema ameridhishwa na viwango vya uzalishaji na ubora wa bidhaa zinazotengenezwa katika Kiwanda cha ALAF Limited, kinachoongoza nchini katika uzalishaji wa mabati na bidhaa nyingine za ujenzi.

Kapinga ameyasema hayo Januri 23 wakati wa ziara ya kukagua shughuli za uzalishaji katika kiwanda hicho, akiwa ameongozana na viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara. Amesema ALAF ni miongoni mwa viwanda vya kuigwa kwa kuwa kimeonesha mfano halisi wa utekelezaji wa dira ya Tanzania ya viwanda.

Amebainisha kuwa ubora wa bidhaa alizoziona unathibitisha uwezo wa viwanda vya ndani kuzalisha bidhaa zenye viwango vinavyokidhi soko la ndani na la kimataifa.

Ameongeza kuwa serikali itaendelea kulinda na kuimarisha mazingira ya biashara kwa viwanda vya ndani ili viweze kuzalisha kwa tija na faida.

Waziri Kapinga pia amepongeza uamuzi wa ALAF kuwekeza katika mtambo wa kisasa wa kuzalisha mabati ya rangi, ulioanza uzalishaji mwaka jana, akisema hatua hiyo imepunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi na kuwezesha watanzania kupata mabati hayo kwa urahisi na kwa wakati.

Ameeleza kuwa uwekezaji huo umechangia kuongeza ajira kwa watanzania na kuimarisha mnyororo wa thamani katika sekta ya ujenzi. Aidha, amesisitiza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya viwanda katika kushughulikia changamoto zinazojitokeza ili kuhakikisha uzalishaji haukwami na kuvutia uwekezaji zaidi.

“Milango ya serikali iko wazi kwa wadau wote. Tunawahimiza mje tujadiliane pale mnapokutana na changamoto ili tuzitatue kwa pamoja na kwa haraka,” amesema.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa ALAF Limited, Bibhu Nanda, alimshukuru Waziri kwa ziara hiyo na kuahidi kuwa kampuni itaendelea kushirikiana kwa karibu na serikali katika kutekeleza malengo ya maendeleo ya viwanda nchini.

Amesema ALAF inalenga kuendelea kuwa kinara katika uzalishaji wa mabati na bidhaa nyingine za ujenzi, akibainisha kuwa ni kampuni kongwe ya mabati nchini inayoadhimisha miaka 63 tangu kuanzishwa kwake.

Nanda amewahimiza watanzania kujivunia na kutumia bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi, hususan za ALAF, kama sehemu ya kuunga mkono jitihada za kukuza uchumi wa viwanda.

ALAF Limited ni miongoni mwa kampuni zinazoongoza nchini katika utengenezaji wa mabati ya kuezekea nyumba na vifaa mbalimbali vya metali vinavyotumika katika shughuli za uezekaji, na imeendelea kuwa mdau muhimu katika maendeleo ya sekta ya ujenzi nchini.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button