Kapinga atoa mwelekeo mpya sekta ya huduma na biashara

DAR ES SALAAM: Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, ametoa mwelekeo mpya unaolenga kuibadilisha sekta ya biashara na huduma nchini, akisisitiza zaidi urasimishaji na uwezeshaji.
Akizungumza leo jijiji Dar es Salaam, katika hafla ya kufunga maonesho ya watoa huduma za sherehe maarufu kama ‘Adorable Wedding Trade Fair’ Kapinga amesema sekta ya huduma ni mhimili muhimu na ajira kwa Watanzania wengi.

Amesema urasimishaji si tu unaleta utaratibu, bali pia unafungua milango ya fursa kwa wafanyabiashara kupata huduma rasmi.
Amesema serikali itafanya juhudi kupunguza udhibiti na kuongeza uwezeshaji, lakini pia kujenga misingi mizuri ya ushirikiano baina ya watoa huduma na Serikali.

“Tukimkuta mfanyabiashara hana ya biashara zake, kwa kuwa ni biashara halali, hatutamfungia biashara, tutamsaidia nini afanye aendelee kubaki katika soko,” amesema Kapinga.
Amesena sekta hiyo itasaidia kukuza soko la ndani na kuimarisha mzunguko wa fedha na Serikali kupata mapato.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Maonesho ya Kibiashara ya ‘Adorable Wedding Trade Fair’, Anna Lema amesema mwaka huu wanatarajia kuandaa ziara ya kibiashara nchini China ili kujifunza zaidi masoko ya kimataifa.

Amesema sekta ya matukio ni pana, inatoa ajira za kutosha, na kuwa na mchango mkubwa katika jamii, na serikali pia.
“Tunaomba serikali itambue rasmi sekta ya matukio na huduma za sherehe kama sekta ya biashara,” amesema Anna.

Amesema kama serikali ikitoa kipaumbele kwa sekta hiyo, ni wazi itaendelea kukuza ajira, na kupongeza mapato serikalini.



