KAPTENI wa jeshi nchini Burkina Faso ametangaza kwenye televisheni ya taifa kwamba amempindua kiongozi wa kijeshi Lt Kanali Paul-Henri Damiba.
Ibrahim Traore alitaja sababu ya Lt Kanali Damiba kutoweza kukabiliana na waasi wa Kiislamu.
Pia alitangaza kuwa mipaka imefungwa kwa muda usiojulikana na shughuli zote za kisiasa zimesitishwa.
Kikosi cha utawala cha Luteni Kanali Damiba kilipindua serikali iliyochaguliwa mwezi Januari, kwa sababu ya kushindwa kusitisha mashambulizi ya Kiislamu.
Lakini utawala wake pia haujaweza kuzima ghasia za wanajihadi. Siku ya Jumatatu, wanajeshi 11 waliuawa walipokuwa wakisindikiza msafara wa magari ya kiraia kaskazini mwa nchi hiyo.
Mapema siku ya Ijumaa, Lt Kanali Damiba aliwataka watu kuwa watulivu baada ya milio ya risasi kusikika katika sehemu za mji mkuu.
Zaidi ya wanajeshi 20 wenye silaha – wengi wao wakiwa wamefunika nyuso zao – walionekana kwenye TV ya serikali muda mfupi kabla ya 20:00 saa za ndani.