Karibu-Kilifair 2025 kuing’arisha sekta ya utalii EAC

JUHUDI za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kujenga sekta moja ya utalii itakayoifanya Kanda nzima kuwa kitovu cha utalii zimezaa matunda kutokana na maonesho ya Karibu-Kilifair 2025.
Maonesho haya makubwa zaidi ya utalii Afrika Mashariki, yanaendelea sasa, yakileta pamoja wajasiriamali zaidi ya 500 kutoka nchi 15 na washiriki wa nje ya nchi zaidi ya 1,000.
Tukio hilo la siku tatu katika Viwanja vya Magereza jijini Arusha, ni jukwaa muhimu kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kuendeleza juhudi zake za kulitangaza eneo hili kama kivutiokimoja cha utalii kupitia chapa ya ‘Tembelea Afrika Mashariki – Feel the Vibe’.
Chapa hii ni mpango wa kimkakati unaolenga kuwaleta pamoja wadau wa utalii wa nchi wanachama wa EAC ikiwa ni pamoja na bodi za utalii, waendesha watalii, wamiliki wa hoteli na watoahuduma ili kukuza ushirikiano wa kuvuka mipaka na fursa.
Tunaamini kuwa Karibu-Kilifair imeendelea kukua kwa miaka mingi, na kuifanya kuwa moja ya maonesho makubwa ya utalii katika ukanda wa Afrika Mashariki na kuvutia idadi kubwa ya wadau wa utalii kutoka pembe zote za dunia.
Tunapongeza juhudi za wadau wote ambao kwa juhudi zao wameifanya sekta ya utalii kuchangia asilimia 17.2 ya Pato la Taifa (GDP) na pia kuchangia asilimia 25 ya mauzo ya nje ya nchi, hivyo kuwa chanzo kikuu cha mapato ya nje kwa nchi wanachama wa EAC.
Kwa kutambua umuhimu wa sekta hiyo muhimu, serikali
imefanya mipango muhimu ikiwamo ‘Tanzania: The Royal Tour’ na ‘Amazing Tanzania’, ambayo imekuwa na athari chanya kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya sekta hiyo.
Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Maliasili na Utalii, mwaka 2024 sekta hiyo ilipata mapato ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 3.9 huku idadi ya watalii ikiongezeka kwa kasi na kufikia zaidi ya milioni 5.3 kwa Tanzania pekee.
Kati ya hao, milioni 2.1 walikuwa wageni na zaidi ya milioni 3.2 walikuwa watalii wa ndani, jambo linaloonyesha wazi kuwa sekta hiyo inaendelea kuvutia watalii wa ndani.
Huu ni ushahidi wa moja kwa moja kuwa sekta ya utalii inakua kutokana na ushirikiano wa pamoja wa kunadi sekta hiyo kutoka nchi mbalimbali wanachama wa EAC.
Wana EAC tunajivunia kuzindua chapa ya utalii ya kikanda yenye umoja, ‘Tembelea Afrika Mashariki – Feel the Vibe’ ambayo ilizinduliwa rasmi kwenye soko la kimataifa mapema mwaka huu huko Berlin.
Ni matarajio yetu kuona sekta hiyo ikikua zaidi sio kwa nchi moja bali kwa nchi zote wanachama wa EAC na kuifanya kuwa chanzo kikubwa cha mapato na fedha za kigeni.