Kasekenya aitaka TANROADS kukamilisha kazi kwa wakati

NAIBU Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya ameutaka Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kubuni mkakati utakaowezesha ujenzi wa barabara na madaraja nchini kukamilika kwa wakati.
Amesema hayo mjini Morogoro wakati akifungua mkutano wa 20 wa baraza la wafanyakazi TANROADS na kusisitiza miradi ikikamilika kwa wakati itapunguza gharama za muda wa nyongeza na hivyo kuleta tija kwa wananchi na Serikali kwa ujumla.
Ameelezea umuhimu wa menejimenti kuwajengea uwezo watumishi kwa kuwapa mafunzo mbalimbali ili wawe wabunifu na wamudu kukabiliana na ukuaji wa mfumo wa teknolojia ya akili mnemba.
Eng. Kasekenya amemuzungumzia umuhimu wa TANROADS kutoa elimu kwa watumishi na wananchi kuhusu utendaji kazi mizani za kupimia magari ili kujenga uelewa wa pamoja na kuondoa malalamiko katika jamii.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la wafanyakazi la TANROADS Eng. Mohamed Besta amesema wamejipanga kuhakikisha wanasimamia miradi ya ujenzi wa barabara na madaraja kwa ufanisi na kushirikiana na wakandarasi ili miradi ikamilike kwa wakati na ubora.
Eng. Besta amesisitiza kuwa na ubunifu, uhusiano na mawasiliano mazuri kati ya memejimenti na watumishi yataendelezwa ili kuleta tija na ufanisi.
Aidha Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Musa Kilakala ameishukuru Serikali kwa ujenzi wa miundombinu ya barabara ya Bigwa-Kisaki KM 78 na Barabara ya Ngerengere-Ubena Zomozi ambapo amesema zitafungua uchumi wa mkoa wa Morogoro na kuipongeza TANROADS kwa kufanya kazi kwa bidii.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi ambae ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu, Mrisho Mrisho, amewataka watumishi wa TANROADS kuwa waadilifu, kufanyakazi kwa kuzingatia miongozo ya Serikali, kutoa huduma bora kwa umma bila upendeleo, kulinda afya zao kwa kufanya mazoezi na kujikinga na maambukizi ya maradhi yanayoepukika.
Mkutano wa 20 wa Baraza la Wafanyakazi wa TANROADS pamoja na mambo mengine unatarajiwa kupitisha mapendekezo ya bajeti ya Wakala huo ya mwaka 2025/26.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button