Katavi wamsifu Samia umeme vijijini

KATAVI: WANANCHI  wa kijiji cha Mapili kilichopo Wilaya ya Mlele, Mkoa wa Katavi wamemshukuru Rais wa Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha kubadili maisha yao kupitia mradi wa umeme uliotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Wametoa shukrani zao kijijini hapo Agosti 13, 2025 kwa nyakati tofauti wakati wa kampeni maalumu ya uhamasishaji wa matumizi ya umeme kwa ajili ya shughuli za kiuchumi inayotekelezwa na REA katika maeneo mbalimbali kote nchini.

“Tunaishukuru Serikali kabla ya kupata nishati hii ya umeme mazingira hayakuwa mazuri, usiku hatukuwa na mwanga sasa hivi tunaishi kwa amani na hata baadhi ya shughuli za maendeleo zinafanyika hadi muda wa usiku,” alisema mkazi wa kijiji cha Mapili, Amos Katawa.

Mrisho Mussa, fundi uchomeleaji katika kijiji hicho amesema kabla ya umeme kufika kijijini hapo wakilazimika kufanya shughuli zao maeneo ya mjini ambapo ni mbali na kijijini hapo hali iliyosababisha kupanda kwa gharama ya bidhaa walizokuwa wakizalisha pamoja na kutumia muda mrefu kukamilisha kazi.

“Tulikuwa tunalazimika kutengenezea mageti huko Inyonga na kisha tunasafirisha, hali hii ilikuwa ni usumbufu kwetu hadi kwa wateja wetu, lakini sasa mambo yote tunafanya hapa Rais Samia ametuona kila kitu hapa hapa kijijini kinapatikana,”amesema fundi Mussa.

Naye Elasto Mwampaya maarufu kama Fundi Lam ambaye ni fundi seremala kijijini hapo alisema kuwa umeme umewezesha kukua kwa karakana yake ya useremala na kwamba hivi sasa anatengeneza fenicha zenye ubora na kuuza katika mikoa mbalimbali kote nchini jambo ambalo halikuwezekana hapo awali kabla ya kufikishiwa umeme.

Ameongeza kuwa umeme umemuwezesha kupanua wigo wa ajira na kwamba katika karakana yake ameajiri vijana wengi na pia anatoa mafunzo kwa vijana wengine namna ya kutengeneza bidhaa kwa kutumia vifaa vya kisasa vinavyotumia umeme.

Akizungumza kuhusiana na umeme kijijini hapo, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Mapili Anthony Mwijuma, aliipongeza REA kwa kutekeleza mradi huo na kusema kuwa ni neema kwa wananchi wake ikilinganishwa na hali ilivyokuwa kabla ya kufikiwa na umeme.

“Wananchi wa Mapili tunasema asante kwa Rais Samia kwani kupitia umeme vijana wamepata ajira, wengine wamebuni miradi na biashara ndogondogo za vinywaji, vifaa vya simu na wengine sasa hivi ni mafundi wa kuchomelea hapahapa kijijini,”amesema Mwijuma.

Akizungumza hali ya usambazaji umeme mkoani Katavi, msimamizi wa miradi ya REA mkoani humo, Gilbert Furia, amesema vijiji vyote vina umeme na kazi inayoendelea sasa ni kusambaza umeme katika vitongoji ambavyo havikufikiwa.

“Tunamshukuru Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha ambayo imewezesha kufikisha umeme katika vijiji vyote 49 ndani ya Halmashauri za Mlele na Mpimbwe na sasa tunatekeleza mradi wa kusambaza umeme vitongojini hadi sasa katika Hamashauri hizi vitongoji 176 kati ya vitongoji 251 vimefikiwa na mradi unaendelea wa kufikisha umeme kwenye vitongoji vilivyobaki,”amesema Furia.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya ya Mlele, Yahaya Mbulu aliipongeza REA kwa kukamilisha mradi wa kufikisha umeme vijijini na kusema  kuwa amejionea namna ambavyo kazi ya kufikisha umeme vitongojini ikiendelea kutekelezwa kwa kasi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button