RUKWA — Polisi mkoani Rukwa wanamshikilia mwanafunzi wa kidato cha nne kwa tuhuma za kumtupa mtoto mchanga chooni muda mfupi baada ya kujifungua, Kamanda wa Polisi Shadrack Masija amesema.
“Mwanafunzi huyo alijifungua kisha kuelekea shuleni kama kawaida,” alisema Masija, akibainisha kuwa mtoto aliokolewa akiwa hai baada ya majirani kusikia kilio chooni.
Tukio hilo limetokea katika Mji wa Namanyere wilayani Nkasi, ambapo mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 18, alidaiwa kutokuwa na ufahamu wakati wa tukio.
“Mama alikiri kutenda kosa hilo akisema hakujua alichokuwa anafanya,” aliongeza Masija.
Mtoto huyo kwa sasa yuko salama na amekabidhiwa kwa mama yake kwa ajili ya kunyonyeshwa, huku uchunguzi wa afya ya akili ukiendelea.