KATAVI: NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Deus Sangu ameupongeza Mkoa wa Katavi kwa usimamizi bora wa fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) na kufuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa miradi inayowanufaisha walengwa wa mfuko huo.
Deus Sangu ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kwela mkoani Rukwa ametoa pongezi hizo leo Novemba 18 katika ziara yake mkoani humo ambapo pia aliwapongeza wanufaika wa Tasaf kwa kushiriki shughuli za kujitolea, zikiwemo ujenzi wa barabara.
“Jambo kubwa lililonileta hapa ni kufuatilia utekelezaji wa fedha za mradi wa Tasaf, mfuko huu umekuwa na programu mbalimbali, zikiwemo zile zinazolenga kaya maskini ambazo hupokea fedha, pamoja na shughuli za kujitolea kama ujenzi wa barabara,” amesema Naibu Waziri Sangu.
Amesema serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, imeanzisha mpango maalum wa kuwasaidia watoto wanaonufaika na Tasaf. Mpango huo unawawezesha wanafunzi waliomaliza darasa la saba kujiunga na vyuo vya ufundi stadi (VETA) bila malipo yoyote.
Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Jamila Yusuph, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko, alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha fedha za Tasaf zinawafikia walengwa na kuboresha maisha yao.
Baadhi ya wanufaika wa Tasaf walieleza jinsi mpango huo ulivyowawezesha kuboresha maisha yao, ikiwemo kujenga nyumba, kusomesha watoto, na kushiriki katika shughuli za maendeleo.
Hata hivyo, Naibu Waziri Sangu alifafanua kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameanzisha mpango wa mikopo yenye riba nafuu kwa vikundi vya wanufaika wa Tasaf, hatua inayolenga kuwawezesha kiuchumi zaidi.