KATIBU Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Gabriel Migire amesema anakitambua kikundi cha wapambanaji cha Mwalu Supporters kinachoundwa na watumishi waliopo taasisi zilizopo chini ya sekta hiyo, kutokana na hamasa inachotoa kwa wachezaji wa klabu ya michezo ya sekta hiyo.
Migire ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam, kikundi hicho kilipokwenda kumtembelea na kuelezea malengo yao katika kufanikisha ushindi katika michezo mbalimbali inayoshiriki klabu hiyo.
Amesema kikundi hicho kimekuwa chachu ya ushindi wa klabu hiyo kwa kutoa zawadi ya fedha taslim kwa wachezaji wanaoshiriki michezo mbalimbali ya Kombe la Mei Mosi Taifa 2023 yaliyokuwa yakifanyika mkoani Morogoro.
“Binafsi nilikuwa nawaona tu kumbe mmekuwa mkifanyakazi nzuri na kubwa sana ya kuwatia hamasa na shime wachezaji wetu, na ninaamini hata ushindi wetu tuliopata nyie mmechangia pakubwa kwa kuweka hamasa ya kutoa fedha kama zawadi, jambo hili muendelee nalo ni jema sana,” amesema Migire.
Amesema kuwa atawapa kipaumbele cha kwanza katika bajeti za michezo ya sekta hiyo kila inapowezekana, maana fedha zinazotumika sasa zinatoka mifukoni mwa wana kikundi hicho, ili kuwapunguzia mzigo.
“Ninahawakikishia kwa kutambua mchango wenu nyie pia mtakuwa sehemu ya wachezaji sio kwamba ni timu pekee bali hata sehemu ya michango, kwa kuwa nyie mnachangia mafanikio ya timu sioni sababu ya nyie kutoa fedha zenu mifukoni kwa hiyo haya mnayoyafanya yanatakiwa yatambulike katika shughuli nzima ya michezo, hata kugawa jezi nao wawe kwenye hesabu,ya kutengewa bajeti, kwani kazi mnayofanya inachangia mafanikio ya klabu,” amesema Migire.
Hatajhivyo, amesema atawasilisha hili kwa kamati ya utendaji ya klabu hiyo, kwa kuwa hakuna sababu ya Mwalu Supporters kutoa fedha zao mifukoni, na watachangia kama kuongezea tu, kwa kuwa siku zote fedha hazitoshi.
Pia amewahakikishia watakuwa pamoja kwa kila wanachofanya kwa ajili ya maendeleo ya klabu hiyo, ikiwemo kuandaa bonanza na marathoni, ila watoe taarifa mapema, ili utekelezaji uwe mkubwa.
Naye Msemaji wa Mwalu Supporters, ambaye pia ni mshereheshaji katika shughuli mbalimbali, Moni Jarufu amesema kuwa kikundi hicho kimeanzishwa kwa lengo la kuwatia hamasa wachezaji wa michezo mbalimbali wa klabu ya sekta ya Uchukuzi wanaposhiriki kwenye michezo, ili waweze kufanya vizuri zaidi.
Amesema ili kutunisha mfuko wao wamekuwa wakijichangisha wenyewe kwa wenyewe na sasa wamepanga kufanya hivyo kwa hiari kila mwezi, na pia wamepanga kufanya marathoni itakayoshirikisha washiriki wengi zaidi na fedha zake zitatumika kuwasaidia wanamichezo wenye vipawa vikubwa lakini hawana uwezo wa kuvionyesha na kukosa vifaa vya michezo.
“Tumefarijika sana Katibu Mkuu umetutambua tunachofanya na ndio maana tumeona ni vyema ukaelewa malengo yetu na yenye nia njema kwa klabu ya sekta yetu, tunaahidi kufanya makubwa zaidi ukiwa kama mlezi wetu unayetutambua, ambapo sasa tutafanya zaidfi ya haya ya kutia hamasa na motisha kwa wachezaji wenzetu wanaoshiriki michezo mbalimbali ikiwemo ya Mei Mosi, SHIMIWI na SHIMMUTA,” amesema Moni.
Mmoja wa waanzilishi wa kikundi hicho, Kenny Mwaisabula ‘Mzazi’, amempongeza Katibu Mkuu kwa kuonesha ushirikiano mkubwa na klabu hiyo, ambapo amekuwa akijitoa kwa moyo kushughudia mechi mbalimbali kipindi cha michezo ya Mei Mosi, bila kujali sikukuu ya Idd pamoja na hali ya hewa ya mvua mkoani Morogoro.
“Tunakushukuru sana kwa kuonesha upendo wa dhati kwa timu yetu pale ulipowahi uwanjani saa 2:00 asubuhi ikiwa ni sikukuu ya Idd na mvua kubwa ilikuwa inanesha lakini ukafika kuwatia moyo vijana wat imu ya soka na michezo mingine na kuangalia mechi yote na tukaibuka na ushindi wa magoli 2-1 dhidi ya Morogoro DC, asante sana,” amesema Mwaisabula.
Mwaisabula ameshukuru pia mchango mkubwa wa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari, ambaye naye alitoa mchango mkubwa kwa kikundi hicho kupitia kwa Juma Kijavara ambaye ni msaidizi wake.