IDADI ya wakazi wanaohamia kwa hiyari kutoka katika Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro kwenda Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, mpaka sasa imefikia kaya 349 ambapo ni sawa na watu 1075.
Takwimu hizo zimetolewa na Mkuu wa wilaya ya Handeni Siriel Nchembe, Wakati akipokea kundi la 12 lenye kaya 61 zenye jumla ya watu 310 walioamua kuhama kwa hiyari katika hifadhi ya Ngorongoro, ili kupisha shughuli za uhifadhi.
Alisema kuwa katika vipindi vya awamu ya kwanza na pili serikali iliweza kujenga nyumba 503, ambazo mpaka sasa nyumba ambazo zimepata watu ni 349.
“Bado Kuna nyumba zaidi ya 100 ambazo zinahitaji watu waweze kuingia na kuishi, hivyo niendelee kuwahamasisha waliobaki waje kwa hiyari Msomera, kwani kuna makazi ambayo yapo tayari kwa àjili yao,”alisema DC Nchembe.
Alisema kuwa serikali imeshaweka mazingira wezeshi, ikiwemo miundombinu ya mabwawa na malambo kwa wananchi hao kuweza kufanya shughuli zao za kilimo, sambamba na ufugaji kulingana na uhitaji uliopo.
“Msomera ni kijiji cha mfano kwa maisha ya wafugaji na wakulima hapa nchini, kwa namna ambavyo serikali ilivyoweza kuweka mazingira mazuri kwa wananchi kuweza kuendeleza maisha yao hapa,”alisema Mkuu huyo wa Wilaya.