DODOMA: MRADI wa Kuwajengea Uwezo Wenye Ulemavu wanaoishi katika Kaya Maskini (DIG) katika Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, umesaidia kuzijengea uwezo kaya 300 za wenye ulemavu kwa kuzipa miradi ya kiuchumi.
Akizungumza jijini hapa baada ya kumsaidia mmoja wa wenye ulemavu kutoka Kijiji cha Majeleko wilayani Chamwino, Melea Obei, Mratibu wa Mradi wa DIG, James Komba alisema mradi huo unalenga kusaidia wenye ulemavu kujikwamua kimaisha.
“Mradi huo uko kwenye kaya 300 ambazo zinaongozwa na wanawake pekee na watu wenye ulemavu, lengo ni kuwainua kiuchumi na kuondokana na hali ya utegemezi kutoka kwa ndugu, jamaa na marafiki,” alisema.
Komba alisema wanufaika wa mradi huo wamepewa mafunzo na kujengewa uwezo wa kuendesha miradi ya kiuchumi ikiwamo ya kufungua maduka, kilimo, ufugaji wa mbuzi, ng’ombe na nguruwe.
SOMA: Serikali inaboresha mazingira wezeshi kwa wenye ulemavu’
Shirika la DIG limewezesha wanufaika hao kwa kuwapatia wanyama wa kufuga pamoja na mitaji ya kufungulia biashara zao. “Baada ya kuwapa mitaji na shughuli za kichumi hatujawaacha hivi hivi, tumewakabidhi kwa walimu wetu ambao watawasimamia na kuwakagua kila mara.
Pia tumewakabidhi kwa mabwana mifugo wa halmashauri ambao watawapatia wanyama chanjo mbalimbali na hata kuwatibu,” alisema.
Komba alisema miongoni mwa wanufaika ni mwenye ulemavu ambaye baada ya kupata ufadhili wa kufunguliwa duka huachana na kuomba misaada kwa watu mbalimbali.
SOMA: https://www.kazi.go.tz/
Mwenye ulemavu huyo wa viungo, Melea mkazi wa Kijiji cha Majeleko wilayani Chamwino, alisema kabla ya kufunguliwa biashara ya duka alikuwa anashinda ndani.
“Nimekuwa hivyo kwa miaka 14, mimi nilikuwa nashinda ndani tu,” alisema na kukiri kuomba kwa wasamaria kutokana na kushindwa kununua madaftari na kalamu za shule kwa ajili ya watoto wake.
Alisema baada ya kupewa mafunzo ya kuwezeshwa kiuchumi, alichagua mradi wa kuuza duka na kufuga bata ambao umebadilisha maisha yake.
Mtendaji wa Kijiji cha Majeleko, Lidya Makasi alisema wanatambua changamoto anazokutana nazo Melea katika kuboresha biashara zake lakini wanashindwa kuboresha mazingira kwa sababu nyumba anayoishi si ya kwake bali kuna msamaria amempa aishi humo.