‘Kazi Iendelee’ yatajwa chachu ya mafanikio
WADAU na wachambuzi wa masuala ya maendeleo wamesema kaulimbiu ya ‘Kazi Iendelee’ inayotumiwa na Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa na mchango chanya katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Wakizungumza na gazeti la HabariLEO wamesema kaulimbiu hiyo imempa Rais Samia Suluhu Hassan ujasiri wa kuwatuliza Watanzania wasilihisi pengo la Dk John Magufuli kutokana na kuyamudu majukumu yote yaliyoachwa na mtangulizi wake.
Mchambuzi wa masuala ya siasa na maendeleo, Abdulkarim Atiki anasema kaulimbiu hiyo imempa ujasiri mkubwa Rais Samia kumaliza viashiria vya uvunjifu wa amani kwa kutumia falsafa ya ‘4R’ katika eneo la maridhiano.
Alisema hatua ya Serikali ya Awamu ya Tano kupiga marufuku shughuli za kisiasa, mikutano ya hadhara na maandamano ilileta tishio la wazi la kupotea kwa amani na utulivu wa nchi, lakini baada ya Rais Samia kuingia
madarakani akawaita wanasiasa wote na kutaka kujenga maridhiano ili nchi iendelee kuwa na amani na utulivu.
“Aliwasihi sana wanasiasa wote kuwa na lugha ya staha wawapo majukwaani ili kutowakwaza wengine hali iliyojenga ustahimilivu baina ya Watanzania kupitia kaulimbiu ya Kazi Iendelee,” alisema Atiki.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino cha Tanzania (SAUT), Dk Kaanaeli Kaale alisema kaulimbinu ya ‘Kazi iendelee’ inafanya kazi vizuri na kuwa kielelezo thabiti cha uongozi uliotukuka wa Rais Samia.
Dk Kaale ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Umma katika Shule ya Habari na Mawasiliano ya SAUT aliongeza kuwa kaulimbiu hiyo iliwarudisha watu katika hali ya kawaida, baada ya kuondokewa ghafla na Dk Magufuli.
Alisema kaulimbiu hiyo iliwajenga Watanzania kisaikolojia kuwa kazi ni lazima iendelee hata baada ya msiba
mkubwa uliolikumba taifa.
Hivyo kaulimbiu hiyo imekuwa chachu kwa Watanzania kufanya kazi kwa bidii ili kutimiza maono ya Rais Samia.
“Kaulimbiu hii imekuwa chachu kwa Watanzania kuunga mkono Serikali ya Awamu ya Sita na imekuwa na matokeo chanya kwa kuendeleza miradi mbalimbali iliyoachwa na Rais Mafuguli pamoja na kuanzisha miradi mingine ili kufanikisha utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa mwaka 2020 – 2025,” aliongeza Dk Kaale.
Alisema kaulimbiu hiyo kwa hakika inatakiwa kuendelea kutumika kwa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya 2025 –
2030 kwa sababu sio kwamba inatia tu hamasa, bali imebeba taswira ya kuona matokeo chanya ya maendeleo endelevu ili kuongeza kipato cha watu waishio kwenye umasikini kuhakikisha wanapata huduma za msingi.
Naye mchambuzi wa masuala ya siasa na uchumi Profesa Humphrey Moshi alisema kukamilika kwa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha kwanza na cha pili pamoja na Bwawa la Nyerere ni ishara tosha inayodokeza mafanikio chanya ya kaulimbiu hiyo.
Alisema kupitia kaulimbiu hiyo, Rais Samia amejenga taifa moja lenye mshikamano linalodumisha amani na utulivu na kwamba baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kaulimbiu hiyo iongezewe maneno isomeke ‘Kazi Iendelee kwa Kasi’.
Mhadhiri wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Zacharia Swedi alisema kaulimbiu hiyo sio tu kumpa ujasiri Rais Samia katika kuendesha serikali, bali pia imewafungua wanawake kuwa hata wao wanaweza, cha msingi ni kusimama imara.
Aliongeza kuwa serikali imefanikiwa kuwajenga Watanzania kuliona suala la kulipa kodi ni suala la kila mmoja hali iliyosababisha mapato ya serikali kuongezeka.
“Kaulimbiu hii imeongeza watalii kupitia filamu ya Royal Tour pamoja na kuongeza idadi ya wawekezaji wanaokuja nchini kuwekeza kutokana na mazingira rafiki yaliyowekwa katika sekta ya uwekezaji,” aliongeza.
Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Ali Khatib aliiambia HabariLEO kuwa kupitia kaulimbiu ya Kazi Iendelee, Rais Samia ameendeleza demokrasia na sekta kilimo, afya, elimu na miundombinu.



