Kidunda: Mabondia tupimwe dawa za kuongeza nguvu

DAR ES SALAAM; Bondia wa ngumi za kulipwa nchini, Selemani Kidunda ametaka mabondia wanaokuja kupigana nchini wapimwe matumizi ya dawa za kuongeza nguvu sababu kuna baadhi wanahusishwa kutumia dawa hizo zisizoruhusiwa michezoni.

Kidunda amesema utaratibu uliopo kwa sasa mabondia wakipigana nchini hawapimwi matumizi ya dawa zisizoruhusiwa michezoni kama wafanyavyo nchi nyingine, badala yake hapa nchini wanapima uzito na afya tu.

“Nilivyopigana juzi na bondia kutoka Afrika Kusini kuna watu walinifuata kwenye kona yangu wakaniambia mwenzako kuna vitu anakula wakihisi labda ni dawa za kuongeza nguvu, sasa baada ya mechi alitakiwa apimwe lakini hapa halifanyiki hilo,” amesema Kidunda.

Amesema utaratibu wa kupima mabondia dawa za kuongeza nguvu dakika kadhaa kabla ya pambano na baada ya pambano, itaongeza chachu ya mabondia kufanya mazoezi zaidi na atapatikana bigwa halali.

Kidunda amesema utaratibu wa kuwapima mabondia wanaokuja kupigana na mabondia wa Tanzania ukifanyika utasaidia na mabondia wa nje kuja nchini kuonesha vipaji na uwezo wao, tofauti na matumizi ya dawa hizo.

“Sisi mabondia wa Tanzania tukienda nchi zilizoendelea kabla ya mchezo na baada ya mchezo unakuja kuchukuliwa kwa lazima na utapimwa kama unatumia dawa za kuongeza nguvu ama la, hapa napo lifanyike hilo,” ameeleza Kidunda.

Kwa sasa Kidunda anatamani kurudiana kupigana na bondia kutoa Afrika Kusini, Asemahle Wellem ambaye pambano lao la kwanza walitoshana nguvu.

Habari Zifananazo

Back to top button