Kifaransa, Kichina na Kiarabu zajumlishwa mtihani darasa 4

BARAZA la Mitihani la Tanzania (NECTA) limesema shule 115 za msingi zimejisajili wanafunzi wake wafanye mitihani ya Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne na ya lugha za Kifaransa, Kichina na Kiarabu.

Katibu Mtendaji wa Necta, Profesa Said Mohamed amesema upimaji huo unafanywa kwa masomo sita nchi nzima leo na kesho.

Profesa Mohamed amewaeleza waandishi wa habari Dar es Salaam kuwa wanafunzi waliosajiliwa ni 1,582,140 kutoka shule 20,517.

“Kwa mara ya kwanza kutakuwa na masomo chaguzi matatu ambayo ni lugha ya Kifaransa, Kichina na Kiarabu na katika hili shule 115 zimejisajili, mwanafunzi ana fursa ya kufanya somo moja tu kati ya hayo matatu,” amesema.

Profesa Mohamed amesema kati ya shule hizo 115, shule 58 zimejisajili kufanya upimaji huo pamoja na somo chaguzi la Kiarabu lakini pia shule 48 kati ya hizo zimejisajili kufanya somo chaguzi la Kifaransa na shule tisa kati ya hizo zimejisajili kufanya somo chaguzi la Kichina.

Amefafanua pamoja na masomo hayo, kuanzia mwaka huu wanafunzi wa darasa la nne watafanya Upimaji wa Kitaifa kwa mara ya kwanza kwa kuzingatia Sera na Elimu ya Mwaka 2014 Toleo la 2023 na mtaala ulioboreshwa.

Amesema katika sera na mtaala huo ulioboreshwa, wanafunzi wa darasa la nne watafanya masomo sita ya msingi ambayo ni Sayansi, Hisabati, (Jiografia, Mazingira, Sanaa na Michezo), Kiswahili, Kiingereza, (Historia ya Tanzania na Maadili).

“Lugha chaguzi zimeongeza idadi ya masomo na kuwa tisa ili kupata kiwango cha ufaulu tutaangalia masomo aliyofanya vizuri zaidi hata kama ni somo la ziada na tutajumuisha kwenye matokeo,” amesema Profesa Mohamed.

Kuhusu upimaji wa darasa la nne SFNA, Profesa Mohamed amesema unaanza kesho na utafanywa kwa siku mbili na wanafunzi waliosajiliwa ni 1,582,140 kutoka shule 20,517, kati yao wasichana ni 817,850 sawa na asilimia 51.69 na wavulana ni 764,290 sawa na asilimia 48.31.

Profesa Mohamed amesema katika watahiniwa hao waliosajiliwa, wanafunzi 1,485,637 sawa na asilimia 93.27 wanafanya upimaji huo kwa lugha ya Kiswahili huku wanafunzi 106,503 wakitarajiwa kuufanya kwa Kiingereza ambao ni sawa na asilimia 6.73.

“Wapo wanafunzi 5,750 wenye mahitaji maalumu kati yao uoni hafifu ni 1,164; wasioona 111; uziwi 1,161; ulemavu wa akili 1,641 na ulemavu wa viungo 1,673,” alisema.

Amesema mtihani wa upimaji wa darasa la pili utafanywa kwa siku tatu kuanzia Novemba 18, 19 na 20.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button