Kihenzile agawa majiko ya gesi jimboni kwake

MBUNGE wa Jimbo la Mufindi Kusini na Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Mwakiposa Kihenzile, ameongoza jitihada za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kugawa majiko ya gesi 2000 kwa mabalozi wa mashina wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika jimbo hilo.

Tukio hili limefanyika katika mkutano maalum uliofanyika katika Kata ya Igowole, Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa na kuhudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, John Mongella.

Katika hotuba yake, Kihenzile alisisitiza umuhimu wa nishati safi kwa ajili ya kulinda mazingira na afya za wananchi.

Advertisement

“Tunafanya hivi kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, za kuhakikisha tunatumia nishati safi. Lengo ni kuepusha madhara yatokanayo na nishati chafu kama ukataji miti holela na magonjwa ya kupumua,” alisema Kihenzile.

Alisema matumizi ya nishati safi ni hatua muhimu kuelekea jamii yenye afya, mazingira endelevu, na maendeleo ya kiuchumi na ni suluhisho linaloendana na juhudi za kimataifa za kulinda mazingira na kuboresha maisha ya watu.

Meneja wa Mauzo wa Kampuni ya Gesi ya Oryx, Alex Wambi, aliungana na Kihenzile kwa kusisitiza umuhimu wa kutumia gesi badala ya kuni na mkaa.

SOMA: Kihenzile Cup: Vijana kazi kwenu

“Gesi inaokoa muda, ni salama, na inaokoa mazingira yetu. Tunapongeza juhudi za serikali na Mheshimiwa Kihenzile kwa hatua hii ya kuwapatia wananchi majiko ya gesi,” alisema Wambi.

Akizungumza katika mkutano huo, Mongella alimpongeza Kihenzile kwa kazi kubwa anayofanya serikalini na wakati huo huo akishughulikia changamoto za watu wake katika jimbo lake.

Aliwataka viongozi wa CCM na wanachama wake jimboni humo kuimarisha mshikamano na kuhakikisha kuwa kazi ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya chama inaendelea kufanywa kwa ufanisi.

“Viongozi wetu kuanzia ngazi ya mkoa, wilaya, kata hadi matawi, wanapaswa kushuka kwenye mashina na kushiriki mikutano inayoeleza mafanikio ya serikali,” alisema.

Alisema mabalozi wa mashina ni uti wa mgongo wa chama hicho na wanapaswa kuungwa mkono ili waweze kutimiza wajibu wao katika kuhakikisha CCM inaendeleakushika madaraka.

SOMA: Kihenzile awaita wawekezaji usafiri wa reli