Atuhumiwa kumbaka ajuza wa miaka 80

JESHI la Polisi Mkoa wa Njombe linamshikilia mkazi wa kijiji cha Mawengi kilichopo Kata ya Kifanya Halmashauri ya Mji Njombe, Otmary Wanderage (38) kwa tuhuma za kumbaka kikongwe mwenye umri wa zaidi ya miaka 80.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Hamis Issa alisema kuwa kijana huyo alimvamia kikongwe huyo na kuweza kutimiza kitendo hicho.

Alisema kijana huyo amekamatwa na upelelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani.

“Watu waache kuwa na tamaa za ajabu ajabu, wewe kijana kwenda kumbaka na kumvamia ajuza wa miaka 80 huo ni unyama wa aina gani? Ni unyama usiovumilika, tunawasihi wananchi msijiingize kwenye uhalifu wa aina yoyote, sheria itafuata mkondo wake na si vinginevyo,” alisema Kamanda Issa.

Katika hatua nyingine, kamanda alisema polisi inawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kujeruhi.

Kamanda alimtaja Baraka Alfonce (20) mkazi wa Kimbila, Ludewa kwa tuhuma za  kumjeruhi mkuu wake wa kazi  , Patrick Mdege (35). Inadaiwa kuwa mtuhumiwa alikuwa akimdai Sh 65,000.

Baada ya kudai na kuona halipwi, alimkata tajiri wake kiganja cha mkono wa kushoto kwa kutumia kitu chenye ncha kali.

Mwingine anayeshikiliwa na polisi ni Grace Kiumbu (30) ambaye ni mkazi wa kijiji cha Idindilimunyo, Halmashauri ya Wilaya ya Wanging`ombe  anayetuhumiwa kumjeruhi baba yake mdogo, Tiles Kiumbu (60) kwa kumkata sehemu za siri na kuziweka pembeni. Ilielezwa kuwa mtuhumiwa ana matatizo ya akili.

 

Habari Zifananazo

Back to top button