Kikongwe agoma kupokea msamaha wa Rais Trump

MAREKANI : MFUNGWA  mmoja nchini Marekani, Pamela Hemphill, aliyehukumiwa kifungo cha siku 60 kwa kushiriki kwenye ghasia za Capitol za Januari 6, 2021, amekataa msamaha kutoka kwa Rais Donald Trump.

Hemphill alieleza kuwa kupokea msamaha kutadhihaki maafisa wa polisi na sheria za nchi, akisisitiza kwamba walikosea siku hiyo na hawapaswi kupokea msamaha.

“Nilikiri mashtaka kwa sababu nilikuwa na hatia, na kupokea msamaha kutachangia tu katika uongo wao na hadithi bandia,” alisema Hemphill.

Hemphill, aliyetajwa na watumiaji wa mitandao ya kijamii kama “Maga granny” kutokana na kuunga mkono kauli mbiu ya Trump ya “Make America Great Again”, alisisitiza kuwa utawala wa Trump ulikuwa ukijaribu “kuandika upya historia,” na hakutaka kuwa sehemu ya hilo.

“Tulikosea siku hiyo, tulivunja sheria na hatupaswi kupewa msamaha,” aliongeza.

Hata hivyo, Rais Trump alitoa msamaha kwa zaidi ya watu 1,600 walioshiriki katika ghasia hizo, hatua ambayo imepingwa na baadhi ya wanasiasa wa chama cha Republican.

Seneta Thom Tillis kutoka North Carolina alisema kuwa hawezi kukubaliana na uamuzi huu, akiongeza kuwa “uamuzi huu unaibua masuala halali ya usalama katika eneo la Capitol Hill.”

Miongoni mwa waliopata msamaha ni Jacob Chansley, maarufu kama “QAnon Shaman,” ambaye aliachiliwa baada ya kutumikia miezi 27 ya kifungo cha miezi 41.

Kwa mujibu wa Katiba ya Marekani, ni haki ya mtu binafsi kukataa msamaha wa rais, na si mara ya kwanza kwa mfungwa kukataa msamaha.

SOMA: Dk Mwinyi asamehe wafungwa wanafunzi 33

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button