Kikwete ataka tofauti za kisiasa zisiyumbishe taifa

RAIS mstaafu, Jakaya Kikwete ametaja mambo sita ya kufanya kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa amani ikiwemo vyama vya siasa kutambua kwamba tofauti za kisiasa hazipaswi kutumika kama sababu ya kuharibu umoja, amani na mshikamano wa kitaifa uliojengwa kwa muda mrefu.

Amevitaka pia vyama vya siasa kufanya siasa kwa amani, vishindane kwa hoja na si kejeli, vitisho, matusi, ugomvi au mifarakano akisisitiza kuwa kuna maisha baada ya uchaguzi.

Kikwete alisema hayo jana wakati akifungua Kongamano la Kitaifa la Sheria lilioandaliwa na Chama cha Mawakili wa Serikali lililofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.

“Tofauti za kisiasa zisitumike kuwa chanzo cha kuharibu umoja wa kitaifa tulioupigania na kuujenga kwa muda mrefu. Mmoja ataahidi maziwa, mwingine ataahidi asali yote yasifanyike katika mazingira ya kuharibu amani, utulivu na mshikamano wa nchi yetu,” alisema

Alisema kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025 ni wakati wa kuonesha uzalendo na kuthibitisha dunia kuwa Tanzania inaweza kufanya mambo yake ya ndani bila ya vurugu na si wakati wa kufanya mzaha kwenye mambo ya msingi kama uchaguzi mkuu.

Alitoa rai kwa vyombo ya ulinzi na usalama na jeshi la polisi kutekeleza majukumu yao kwa weledi kwa kulinda haki za kisiasa za raia.

Aliitaka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kufanya kazi kwa weledi, uwazi na uhuru huku akiwataka wananchi na vyama vya siasa kuwa na imani na Inec ili uchaguzi ufanyike kwa utulivu na nchi iwe tulivu.

Aliitaka mahakama na vyama vya kisheria vilivyopewa mamlaka ya utatuzi wa malalamiko yahusuyo mchakato wa uchaguzi watekeleze majukumu yao kwa kufuata sheria asimamie sheria.

Kikwete alihimiza wananchi kupatiwa elimu juu ya umuhimu wa kushiriki uchaguzi kwa amani na wahamasishwe ili kutekeleza wajibu wao wa kikatiba.

Alisema ni muhimu kila mtu kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa sheria katika demokrasia na uwajibikaji.

Alisema mchakato wa uboreshaji wa sheria ni endelevu na umekuwa ukifanyika katika kila awamu ili kuleta ufumbuzi wa changamoto za wakati huo katika uchaguzi na kuboresha mchakato mzima wa uchaguzi.

Alisema uboreshaji wa sheria za uchaguzi hasa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya 2024 na Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya 2024  umeongeza uwazi na demokrasia.

Kadhalika, Kikwete alisema baadhi ya watu wamekuwa wakitoa taarifa za upotoshaji kwa maslahi yao binafsi kuhusu uboreshaji wa sheria uliofanyika kwa madai mbalimbali.

“Kuna wakati mwingine kuna watu wanataka kufanya lolote, mahali popote hata kama litavunja sheria lakini wote mseme ndio wakati mwingine matatizo haya ni ya wanasiasa… sasa sheria hazijaenda likizo ni muhimu kila mmoja akatimiza wajibu wake,” alisema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button